Tuesday 13 August 2013

UUNGWANA NI VITENDO.

Ibrahim Boubacar keita
 Ibrahim Boubacar Keita, rais wa Mali aliyeshinda katika duru ya pili ya uchaguzi nchini humo.

Uchaguzi wa urais wa duru ya pili nchini Mali.

  • Soumalia Cisse aonesha uungwana, akubali matokeo
  • Asema bwana Keita alishinda uchaguzi huo kihalali
  • Amfuata bwana Keita nyumbani kwake kumpongeza



            Na. deo kaji makomba,  

                    na mashirika ya habari.



Mgombea urais nchini Mali, Soumalia Cisse ameonesha uungwana kwa  kukubali kushindwa na mpinzani wake Ibrahim Boubacar Keita katika duru ya pili ya uchaguzi  uliofanyika Jumapili, nchini humo.

Akizungumza Jumatatu  jioni Cisse alisema bwana Keita alishinda uchaguzi huo kwa njia halali na kumtakia kila la kheri.

Msemaji wa bwana Keita, Mamadou Camara ,alisema matokeo yanaonyesha kuwa, alipata kati ya asili mia 70 na 80 ya kura.


Camara alisema bwana Cisse alimtembelea Keita nyumbani kwake Jumatatu jioni na kumpongeza kufuatia ushindi huo.

Aidha, Jumanne hii, msemaji huyo  alisema kuwa ushindi wa bwana Keita ulikuwa mkubwa na kwamba sasa ataelekeza nguvu zake zote katika kuleta maridhiano ya kitaifa nchini Mali.

HAKUSHIKIKI HUKO MISRI


Wandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani huko nchini Misri Bwana Mohamed Morsi, wakirushiana mawe na wale wanaounga mkono kuondolewa madaraki kwa kiongozi huyo.


Ni mshikemshike huko nchini Misri.


  •  Polisi watumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa morsi
  • Chupa na mawe vatumika kushambuliana  kati ya wafuasi wa morsi na wapinzani wake.


                Na. deo kaji makomba

                     na mashirika ya habari


Polisi nchini Misri, wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani, Mohammed Morsi wakati wa maandamano yao mjini Cairo.
Vikosi vya usalama viliingilia kati maandamano hayo baada ya wafuasi wa Morsi   kukabiliana na wapinzani  wao wa kisiasa.
Bwana Morsi, aliondolewa madarakani na viongozi wa jeshi mwezi Julai mwaka huu, kufuatia maandamano makubwa.

Walioshuhudia vurugu hizo wamesema kuwa wafuasi wa bwana Morsi na wale  wanaounga mkono serikali ya mpito walirushiana mawe na chupa huku watoto na wanawake wakikimbia kuokoa maisha yao.
Kutokana na ghasia hizo, jeshi nchini Misri limeweka serikali ya mpito.
Wafuasi wa Morsi aliyeingia madarakani baada ya vuguvugu la kiisilamu la Brotherhood kushinda uchaguzi wa rais, wanakataa kukubali serikali mpya ya mpito wakisisitiza kuwa lazima rais wao arejeshwe madarakani.


Vurugu za Jumanne hii zilianza wakati wafuasi wa Morsi, walipotembea hadi sehemu moja ya Cairo ambako watu wengi wanapinga vuguvugu la Muslim Brotherhood.
Waandamanaji hao walijaribu kuingia katika ofisi za wizara moja ingawa polisi waliwalazimisha kuondoka kwa nguvu.
Wakaazi wa eneo hilo walianza kuwakejeli waandamanaji na hapo ndipo polisi walipoingilia mzozo huo.

Mamilioni ya wamisri waliandamana kumtaka Morsi aondolewe mamlakani ingawa wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kuondolewa kwake kunaonekana kuzorotesha migawanyiko ya kisiasa iliyoko kwa sasa.


Wafuasi wake wamekuwa wakipiga kambi mjini Cairo wakitaka arejeshwe mamlakani, ilihali kiongozi wao akiwa kizuizini huku nchi hiyo ikiwa katika serikali ya mpito.

Maafisa wa usalama walitishia kuondoa mahema waliyoweka wafuasi wa Morsi ambako wamekuwa wakipiga kambi lakini wakabatili uamuzi wao baada ya kuamua kuuakhirisha.


KUELEKEA MSHIKEMSHIKE WA LIGI KUU YA SOKA YA ENGLAND.




Marouane chamakh “aikacha” Arsenal na kukimbilia Crystal Palace

Na. deo kaji makomba

Huko nchini England klabu cha kandanda cha Crystal Palace kimefanikiwa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Morocco, Marouane Chamakh kwa mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Morocco mwenye umri wa miaka 29, atakuwa akivaa jezi namba 29 mgongoni, baada ya kukamilisha mchakato wa kuchukua vipimo vya kitabibu.

Awali Chamakh alisaini mkataba na washika bunduki hao wa London, Asernal the Gunner mnamo mwaka 2010, akijiunga na klabu hiyo kwa uhamisho wa bila malipo kutoka klabu cha kandanda cha Bordeaux, lakini baada ya kufunga magoli 11 wakati akiwa katika mwaka wake wa kwanza huko London.

Shamakh alitolewa kwa mkopo kwenda West Ham hapo mwezi januari mwaka huu, lakini alicheza mechi tatu.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Morocco, ni mshambuliaji wa tatu ambaye amesajiliwa katika msimu huu wa kiangazi, akiungana na Kevin Philips aliyesajiliwa bila malipo pamoja na Dwight Gayle kutokea Peterborough

Vijana hao wa Ian Holloway’s wataanza kampeni zao za kuwania ubingwa wa ligi kuu ya soka ya England jumapili hii.

“HATUNA IMANI NA UCHUNGUZI WA PONDA”








Tukio la kupigwa risasi kwa shekh Mponda

·        Watetezi wa haki za binadamu na taasisi mbalimbali za dini, walaani tukio hilo.


·        Wasema hawana imani na uchunguzi kuhusu Mponda


 


        Na. Mwandishi wetu 

                 Dare es salaam.



 

Tukio la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi mkoani Morogoro kimeamsha hisia tofauti miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu na taasisi mbalimbali za dini nchini Tanzania na kuongeza kuwa hawana imani na uchunguzi kuhusu shekh Mponda.

Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania kupitia kituo cha sheria na haki za binadamu Tanzania pamoja na kulaani tukio la kujeruhiwa kiongozi huyo wa taasisi ya kiisalam wametaka tume ya haki za binadamu na utawala bora nchini kufuatilia pia matukio mengine ambayo inadaiwa  vyombo vya dola vinatumika kuua na kujeruhi raia.

Wakati jeshi la Polisi nchini likitangaza kuundwa kwa timu ya maafisa polisi kupitia timu inayojulikana kama haki jinai, watetezi wa haki za binadamu wamepinga hatua hiyo kwa madai kwamba polisi hawawezi kujichunguza wenyewe.

Nalo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)  kwa upande wake limelaani kitendo cha kujeruhiwa kiongozi huyo  wa kikundi cha kiislamu ambaye anadaiwa kutafutwa kutokana na tuhuma za uchochezi baada ya kupewa kifungo cha nje na mahakama moja huko jijini Dar es salaam.

Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Alhad Mussa Salum amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kwamba iwapo Polisi mkoani Morogoro wamehusika na kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda, basi wamefanya kitendo kibaya ambacho kinaondoa imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Akizungumzia  uhusiano wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania na Taasisi inayoongozwa na Sheikh Ponda, ambayo inadaiwa kutotambuliwa,  Alhad Mussa amesema Bakwata  haina uadui na Sheikh Ponda kiasi cha kumtaka adhurike.
Shekh Mponda Issa Mponda pichani akionekana katika jukwaa akitoa muhadhara

Naye kamanda wa kanda maalum ya kipolisi Dar es salaam Suleiman Kova alithibitisha kujeruhiwa na kulazwa kwa shekhe Ponda katika taasisi ya mifupa MOI jijini Dar es alaam huku akitaka masuala mengine yanayohusiana na kukamatwa kwake kuachiwa kamanda wa polisi mkoani Morogoro.

Akiwa mkoani Morogoro juzi Sheikh Ponda Issa Ponda alijeruhiwa begani na kitu kinachodhaniwa ni risasi wakati Polisi mkoani humo walipokuwa kwenye harakati za kumkamata.


.Awali siku ya Jumapili Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Tanzania, Alhajj Mussa Kundecha, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya nchi hiyo.

Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya Taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.

Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.