Tuesday 29 October 2013

IMANI ZA KISHIRIKINA ZAENDELEZA UNYAMA KWA BINAADAM.





 Wanaoonekana katika picha watu wawili ambao majina yao yamehifadhiwa, wakiwa na mkono wa binadamu(Picha na mpiga picha wetu.)
Biashara ya viuongo vya binadamu bado yaendelea mikoa ya kanda ya ziwa.

  • Polisi mkoani Mwanza wafanikiwa kukamata watu watatu wakiwa na kiungo cha binaadamu.

  •  Kilikuwa kikiuzwa kwa gharama ya shilingi milioni 100.

                        
                                       Na. Mashaka Baltazar.

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza,linawashikilia waganga wa jadi wawili na mkulima mmoja, baada ya kuwakamata wakiwa na kiungo cha binadamu,wakitaka kukiuza kwa shilingi milioni 100.

Watuhumiwa hao walikamatwa juzi Oktoba 28 mwaka huu, majira ya saa 9 alasiri eeneo la ziwani jirani na uwanja wa Ndege wa Mwanza katika Manispaa ya Ilemela.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai (RCO) na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Kamishna Msadizi wa Polisi, Joseph Konyo,alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kupata taarifa na kuwafuatilia.

Alisema Oktoba 20 mwaka huu,walipata taarifa kuwa mtu mmoja alikuwa akijihusisha na biashara ya viungo vya binadamu katka eneo la Igombe Manispaa ya Ilemela.

Kwamba baada ya taarifa hizo, jeshi la polisi lilimtuma mtu wake kwa ajili ya kufanya manunuzi ya viungo hivyo, kutoka kwa mganga mmoja (jina linahifadhiwa)

“Hivi karibuni tulifanya vikao na waganga wa jadi kuzungumzia umuhimu wa kushirikiana na kupeana taarifa za kubaini waganga wanaopiga lamli chonganishi na wakata mapanga, Lengo likiwa ni kukomesha mauaji ya vikongwe,”alisema ACP Konyo na kuongeza;

“Oktoba 20, mwaka huu baada ya vikao tulipokea taarifa kuwa mganga wa jadi huko Igombe anauza viungo vya binadamu. Tulimtuma mtu wetu akiomba kununua,ambapo mganga huyo aliweka muda maalum wa kuleta kichwa cha binadamu,mkono na nyeti.”

Alieleza kuwa kikosi cha jeshi hilo kikiwa kazini mganga huyo aliwaarifu kuwa amekamilisha kazi hiyo, hivyo wakutane kwa ajili ya kufanya biashara na kudai kuwa angeambatana na watu wengine wawili na akapanga mahali pa kukutania.

“Alituarifu kuwa anavyo viungo hivyo tukamfuata mahali tulipokubaliana . Tuliwakuta wote watatu  wakiwa na begi ambapo,mganga huyo alitaka apewe shilingi milioni 100 mtu wetu akaomba apunguze bei ndipo tukawaweka chini ya ulinzi,”alisema

Alisma walipowapekuwa ndani ya begi hilo walikuta kukiwa na chungu na ndani ya chungu kulikuwa na mfuko wa plastiki na ndani ya mfuko huo kulikuwa na mwingine mweupe wa nailoni ndani yakee wakakuta kiganhja cha mkono wa kuume wa bnidamu.

“Tuliwaweka chini ya ulinzi na tukafuata taratibu za upekuzi. Katika upekuzi ndani ya begi lao tulikuta chungu ambacho ndani yake kulkuwa na mfuko mweusi,ndani ya mfuko huo kulikuwa na mfuko wa nylon, mweupe ambao tuliukuta ukiwa na kiganja cha mkono wa kulia wa binadamu kikiwa hakijaharibika na walituonyesha ni  binadamu gani,”alisema ACP Konyo

Hata hivyo alikataa kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa madai ya kuvuruga upelelezi, kwa kuwa bado wanamtafuta mfanyabiashara mmoja wa jijini hapa,baada ya kutajwa na watuhumiwa kuwa anajihusisha na biashara hiyo ya viungo vya binadamu.

Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mauaji ya kinyama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi albino nchini Tanzania, huku ikielezwa kuwa mauji hayo yamekuwa yakifanywa kutokana na imani potofu za kishirikina kuwa kiuongo cha binadamu mwenye ulemavu wa ngozi ya albino kinaweza kuwapatia utajiri.

Hadi hivi sasa serikali ya Tanzania pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekuwa yakipambana na mauaji hayo ya kinyama ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa wa mauaji hayo pamoja na kuwafikisha mahakamani na hukumu kutolewa.