Friday 18 October 2013

NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA NYASI KUWAKA MOTO WEEKEND HII



 Mashabiki wa timu ya soka ya Yanga wakiwa katika hemwahemwa.

Harakati za kuwania ubingwa wa ligi kuu soka ya bara.

·      Weekend hii ni patashika nguo kuchanika viwanjani.
·         Patashika hiyo kuanza jumamosi hii na kumalizikia jumapili kwa mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga.


                                     Na. Deo kaji Makomba.


Hekaheka za kuwania ubingwa wa ligi kuu soka ya Vodacom Tanzania bara, zinatarajia kuendelea weekend hii huku kukishuhudiwa mechi kadhaa zikipigwa katika viwanja tofauti.

 Timu mbalimbali  zitapambana kuwania pointi tatu muhimu ili kuweza kujiweka kwenye mazingira mazuri katika harakati hizo za kuwania ubingwa wa ligi hiyo ya Tanzania bara.

Jumamosi hii kivumbi cha ligi  Kuu ya Vodacom (VPL) kitaendelea kutimka kwa mechi tano huku Mbeya City ikiikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Oljoro JKT na Azam (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Mtibwa Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Manungu, Turiani), Ashanti United na Ruvu Shooting (Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam) na Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba).

Licha ya michezo hiyo jumamosi hii, mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga utakaopigwa jumapili hii ndio umekuwa gumzo kubwa miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini Tanzania, kutokana na timu hizo kuwa na ubipanzani mkubwa pindi zinapokutana uwanjani.


 Picha ikionesha kikosi cha wachezaji wa timu ya Simba cha mwaka wa 2010

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na na nakala yake kukifika kisima chetu cha habari, imeeleza kuwa, Mechi hiyo baina ya Simba na Yanga itaanza majira ya saa 10 kamili jioni.

Ama kwa hakika mchezo huo utakuwa wa vutanikuvute kutokana na kila timu kutaka kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi kuu hiyo lakini pia kila moja ikitaka kuonyesha utemi kwa mwenzake.

Katika msimu uliopita, wekundu wa Msimbazi Simba walikubali kichapo kutoka kwa watani wao wa jadi Yanga, katika katika mchezo wa marudiano wa ligi hiyo.

MAJINA YA WAGOMBEA WA TFF



Kuelekea mkutano mkuu wa uchaguzi wa TFF.
·      Kamati ya uchaguzi ya shirikisho hilo, yaweka hadharani majina ya wagombea wa uchaguzi huo.
·        Majina ya wanaogombea katika bodi ya ligi nayo yatangazwa.

           
         Na. Mwandishi wetu, Dare es salaam.


Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza orodha ya mwisho ya wagombea wa uchaguzi wa TFF na wa Bodi ya Ligi (TPL Board) utakaofanyika baadaye mwezi huu.

Uchaguzi wa Bodi ya TPL utafanyika Oktoba 25 mwaka huu wakati ule wa TFF utafanyika Oktoba 27 mwaka huu.

 Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa TPL Board na ule wa TFF zimeanza ijumaa hii (Oktoba 18 mwaka huu)  zitamalizika siku moja kabla ya uchaguzi saa 10 kamili alasiri.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni amewataja wagombea kwa upande wa TPL Board kugombea uenyekiti ni Hamad Yahya Juma (Mtibwa Sugar), Makamu Mwenyekiti ni Said Muhammad Said Abeid (Azam).

Wanaowania ujumbe wa Bodi ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo (Pamba) na Omary Khatibu Mwindadi (Mwadui).

Wagombea kwenye uchaguzi wa TFF ni Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emily Malinzi (Rais), Imani Omari Madega, Ramadhan Omar Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais).

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera), Jumbe Odessa Magati, Mugisha Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Lufano (Kanda namba 2- Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu).

Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii Ali (Kanda namba 4- Arusha na Manyara), Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo (Kanda namba 5- Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo (Kanda namba 6- Katavi na Rukwa), Ayoub Shaibu Nyenzi, David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve, Lusekelo Elias Mwanjala (Kanda namba 7- Iringa na Mbeya).

James Patrick Mhagama na Stanley William Lugenge (Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma), Athuman Kingombe Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder (Kanda namba 9- Lindi na Mtwara), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima, Charles Komba (Kanda namba 10- Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala) na Twahil Twaha Njoki (Kanda namba 11- Morogoro na Pwani).

Davis Elisa Mosha, Khalid Abdallah Mohamed (Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani), Alex Crispine Kamuzelya, Kidao Wilfred Mzigama, Muhsin Said Balhabou na Omary Isack Abdulkadir (Kanda namba 13- Dar es Salaam).

Mbwezeleni amewataka wagombea kufanya kampeni bila kukashfu wenzao, kwani Kanuni ya Uchaguzi za TFF toleo la 2013 inatoa fursa kwa Kamati ya Uchaguzi kuwaondoa wagombea wa aina hiyo kwenye uchaguzi.