Tuesday 22 October 2013

YANGA WALOANISHWA DAKIKA AROBAINI NA TANO ZA MWISHO.



Haruna Niyonzima wa Yanga mwenye mpira akijaribu kumtoka Nassoro Cholo wa Simba wakati wa mpambano wao jumapili iliyopita.

Kutangulia sio kufika.

· Simba yatoka nyuma na kusawazisha.
· Yanga yashindwa kulinda mabao yake uwanja wa taifa.
· Mamilioni ya shilingi yapatikana kutokana na viingilio.
                       Na. Mwandishi wetu.

Ule usemi usemao kutangulia si kufika umedhihirika jumapili iliyopita, wakati watani wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga walipokuwa wakipepetana katika moja ya mechi ya harakati za kuwania ubingwa wa ligi kuu soka ya Vodacom Tanzania bara.

Kudhihirika kwa usemi huo, kunafuatia timu ya Yanga iliyokuwa mbele kwa magoli 3 – 0 dhidi ya Simba, iliyoyapata katika kipindi cha kwanza, kushindwa kuyalinda na hatimaye Simba kusawazisha mabao hayo, katika mchezo wa ligi kuu ya soka ya Vodacom uliopigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dare es salaam, jumapili iliyopita.

Alikuwa ni mchezaji Mrisho Khalfan Ngassa, aliyewainua wapenzi na mashabiki wa timu yake kwa kuandika bao la kwanza, huku mchezaji Hamis Kiiza akipachika bao la pili na la tatu na hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko huku ikiwa mbele kwa mabao hayo 3 – 0 dhidi yawekundu wa Msimbazi Simba.

Kwenye kipindi cha pili Simba walichachamaa na kuweza kuutawala mchezo huo katika kipindi hicho na hatimaye kuweza kupata mabao hayo ya kusawazissha yaliyoamsha hoi hoi na ndelemo kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.

Mchezaji Bitlam Mombeki wa Simba aliipatia bao la kwanza timu yake naye mganda Joseph Owino akiifungia Simba bao la pili wakati bao la tatu la Simba likpachikwa wavuni na Gilbert Kaze.

Jumla ya shilingi 500,727,000 zimepatikana kutokakana na viingilio vya mlangoni katika mchezo huo uliopigwa jumapili iliyopita.

Kwa matokeo hayo sasa Simba wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu hiyo kwa kuwa na pointi 19 kibindoni wakati Yanga wao wakiwa na pointi 16 na hivyo kushikilia nafasi ya Nne.

Azam FC ndiyo iko kileleni mwa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 20 ikifuatiwa na Mbeya City inayoshikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.