Wednesday 6 November 2013

KINA DADA WA TANZANITE WAKIPASHA MISULI MOTO KABLA YA KUELEKEA MSUMBIJI



Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite, kikipasha misuli moto, kabla hakijaelekea Maputo, Msumbiji.
TANZANITE YAELEKEA  MAPUTO MSUMBIJI.


                             Na. Mwandishi wetu.

Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) imeagwa jana jumatano (Novemba 6 mwaka huu) saa chache kabla ya kuanza safari ya kwenda Maputo, Msumbiji.

Hafla fupi ya kuikabidhi bendera Tanzanite imefanyika jana jumatano saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF wakati kikosi hicho  kikiondoka saa  saa 11 jioni kwa ndege ya LAM na kuwasili Maputo saa 3.45 usiku.

Msafara wa Tanzanite ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 10-0 karibu wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Kidao Wilfred.

Mechi hiyo ya marudiano itachezwa Novemba 9 mwaka huu Uwanja wa Taifa wa Zimpeto, na timu itarejea nyumbani Novemba 10 mwaka huu saa 8.30 mchana kwa ndege ya LAM.

ORODHA YA WALIOPATA MSAMAHA WA RAIS WA TFF YATAKIWA



 Rais mpya wa TFF, Jamali Malinzi 
TFF YATAKA ORODHA YA WALIOSAMEHEWA.
·    Ni kufuatia msamaha wa rais mpya wa shirikisho hilo.
·    Vyama vya soka ngazi ya wilaya, mkoa na vyama shiriki kuwajibika katika hilo.

                
                         Na. Mwandishi wetu.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limevitumia waraka  vyama vya mpira wa miguu vya wilaya, mikoa na vyama shiriki kuvitaka kuwasilisha orodha ya wote waliofaidika na msamaha wa Oktoba 28 mwaka huu.

Taarifa hiyo ya TFF kuvitumia waraka vyama vya soka vya wilaya, mikoa na vyama shiriki kuhusiana kutaka orodha ya waliosamehewa katika msamaha wa rais wa TFF, imetolewa na kaimu katibu mkuu wa shirikisho hilo, Boniphace Wambura.

Oktoba 28 mwaka huu wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu mara  baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, Rais mpya wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi alitoa msamaha kwa wote waliofungiwa kwa sababu mbalimbali.

Taarifa hiyo iliyotolewa na TFF, imesisitiza kuwa, msamaha huo hauwahusu waliofungiwa kutokana na makosa ya rushwa au kupanga matokeo.  Vilevile haugusi adhabu zilizotolewa ndani ya klabu.

Vyama vya mikoa vinatakiwa kuhakikisha waraka huo unafika kwa wanachama wao (vyama vya mpira wa miguu vya wilaya). TFF inataka orodha ya wote waliofaidika na msamaha huo kwa ajili ya kumbukumbu zake (records).