Saturday 16 November 2013

DROO YA MAKUNDI YA CECAFA CHALENJI YAFANYIKA NAIROBI KENYA.



 Nicholas Musonye, katibu mkuu wa CECAFA.
Makundi ya CECAFA chalenji Cup yatangazwa huko Nairobi.
·    Tanzania yapangwa kundi moja na Zambia.
·    Ratiba ya michuano hiyo kuwekwa hadharani wiki ijayo.

                              Na. Deo Kaji Makomba.

Droo ya makundi ya timu za taifa zitakazocheza katika michuano ya kuwania kombe la CECAFA chalenji mwaka huu huko nchini Kenya imefanyika hapo jana ijumaa mjini Nairobi huku kila timu ikipangwa katika makundi tofauti.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na shirikisho la soka kwa nchi za Afrika Mashariki na kati CECAFA na nakala yake kukifikia Kisima hiki cha habari, imeeleza kuwa makundi ya A, B na C yameundwa kuelekea mashindano hayo yanayotarajia kuanza kurindima hapo Novemba 27 mwaka huu huko mjini Nairobi nchini Kenya.

Kulingana na taarifa hiyo, kundi A lina timu mwenyeji Kenya, Ethiopia, Zanzibar pamoja na Sudani ya kusini wakati kundi B Tanzania, Zambia, Burundi pamoja na Somalia zimepangwa katika kundi hilo.

Kulingana na taarifa hiyo, timu za Uganda, Rwanda, Sudani na Eritrea zimepangwa katika kundi C na ikielezwa kuwa ratiba ya michuano hiyo itawekwa hadharani wiki ijayo.