Monday 28 October 2013

HATIMAYE RAIS MPYA WA TFF APATIKANA



Rais mpya wa shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, Jamali Malinzi.
Malinzi ndiye rais mpya wa TFF.

  •      Atoa msamaha kwa waliokuwa wamefungiwa katika masuala ya soka.

  • Nafasi ya ujumbe kwa kanda ya ziwa, Nyalla nje, Lufano ndani.


                     Na. Mwandishi wetu.

Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Malinzi ameshinda wadhifa huo katika uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya TFF uliofanyika juzi (Oktoba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa miguu nchini unasonga mbele.


 Rais wa TFF aliyemaliza muda wake Leodiga Chila Tenga, akimkabidhi mpira rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi mpira baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa TFF jumapili iliyopita
Rais mpya wa TFF, Jamali Malinzi akiwa na kamati kuu mpya tendaji ya shirikisho hilo.

Pia ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu zilizotolewa katika ngazi ya klabu.

Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).

Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni  Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).

Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.

Ayubu Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).

Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).

Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).

Kanda namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha.  Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).

ROCK CITY MARATHON YAFANYIKA JIJINI MWANZA




Msanii wa kikundi cha Utamaduni cha Cecilia cha Bujora, akicheza na nyoka aina ya chatu. Alikutwa jana kweny uwanja wa CCM Kirumba wakati wa mbio za Rocky City Marathon.
Klabu ya riadha kutoka mjini Moshi mkoani Kilimanjaro yatamba Rock city Marathon.

                           Na. Mashaka Baltazar.

WAFUKUZA upepo wa Klabu ya Riadha ya Holili Youth Athletics ya Moshi (HYAC), wameitoa kimasomaso Tanzania, katika mashindano ya mbio ndefu za Rocky City Marathon.

Katika mashindano hayo ambayo yalifanyika jijini Mwanza jumapili iliyopita, wanariadha wa klabu hiyo walishika nafasi ya kwanza, ya pili kwa mbio za Kilomita 21 wanaume na kuwashinda wapinzani wao wakiwemo raia wa Kenya,ambapo Sara Ramadhani alishika nafasi ya pili kwa wanawake.

Akizungumza na Kisima cha habari kuhusiana na ushindi huo, Mkurugenzi wa Holili Youth,Domician Rwezaura, alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi na mazoezi ya wanariadha wa klabu hiyo pamoja na kujituma.

Alisema baada ya kutofanya vizuri mwaka jana walijipanga na kufanya mazoezi  wakilenga kulinda vipaji vyao lakini pia kujiandaa na mashindano mbalimbali.

“Ni ushindi wa kujivunia ukizingatia Rock City Marathon ni mashindano ya Kimataifa,yanayoshirikisha wakiambiaji kutoka nje ya  nchi. Ingekuwa aibu kwa Tanzania zawadi zote za kwanza kunyakuliwa na wageni,”alisema Rwezaura

Alitoa rai kwa waandaaji wahamasishe mchezo wa riadha nchini badala ya kuangalia mapato, kiwezkana wadhamini nao kwa upande mwingine wajitokeze kuhammasiha jamii kuupenda na kuthamini mchezo huo.

Mwanariadha Alphoncce Alex wa Holili,alishika nafasi ya kwanza mbele ya Mkenya Joel Kimtae ,akitumia muda wa saa 1:02:17 na kuuvunja rekodi ya mwaka jana ya saa 1:04 iliyowekwa na Dickson Marwa.

Nafasi ya tatu mbio hizo za Kilomita 21 ilinyakuliwa na Sambu Andrew wa Holili.Upande wa wanawake nafasi ya pili ilitwaliwa na Sara Ramadhan wa Holili, nyuma ya Victoria Chepkemoi wa Kenya,ambapo Zakia Mrisho alishika nafasi ya tatu na wanne alikuwa na Damaris Aleba.

Wambura Lameck wa Holili alishika nafasi ya kwanza kwa wanaume,wa pilii Dottto Ikangaa na wa tatu alikuwa ni Juma Nyang’au, mbio za Km 5, huku Neema Mathias pia wa Holili akishika nafasi ya pili.

Mshindi  wa kwanza wanaume mbio za km 21,alizawadiwa sh.1.5 milioni na tiketi ya ndege, wa pili sh.900,000 na king’amuzi na watatu alipata sh.700,00 na king’amuzi.

Kwa upande wa wanawake zawadi zilikuwa sh.1.5, wa pili sh.900,000 na king’amuzi,wa tatu sh.00,000 na kingamuzi,ambapo washiriki wengine walioshika nafasi ya nne hadi ya kumi walipata kifuta jasho.

Wadhamini wa mashindano hayo Kampuni ya mawasiliano ya Airel na mfuko wa hifadhi ya Jamii, (NSSF) kwa nyakati tofauti walisema mashindano ya mwaka huu yamekuwa na hamasa kubwa kutokana na washiriki wengi kujiokeza.

“Mashindano haya yako katika ngazi ya Kimataifa na yamekuwa na hamasa kubwa mwaka huu,yamevuta washabiki wengi ambapo yameshirikisha  watoto, wazee na watu wenye ulemavu,”alisema Jackson Mbando..

“NSSF tumekuwa wadhamini wa Rock City Marathon tangu miaka mitano Iliyopita, pamoja na kuwa na  mafao ya ulemavu kazini ,lakini tumelenga kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kushiriki riadha na kuibua vipaji,”alisema Eunice Chiume,Meneja Mawasiliano Kiongozi wa NSSF

Mashindano ya mwaka huu ambayo yalikuwa ya umbali wa km 2.5,km 5 na km 21 yalishirikisha watoto wa umri wa miaka 7 hadi 10,wazee,walemavu wafanyakazi wa taasisi mbalimbali na wanariadha wnye umrii tofauti tofauti.