Sunday 16 June 2013

SIOGOPI IVORY COST , ASEMA POULSEN.


    Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, taifa stars Kim Poulsen akizungumza na wandishi wa habari jiji Dar es salaam.

Na. Deo Kaji makomba.
 
Wakati timu ya soka ya Tanzania,Taifa stars ikishuka uwanjani hii leo kupepetana na Ivory Cost, kocha mkuu wa Stars Kim Poulen, amesema kuwa kamwe haiogopi Ivory Cost na kwamba vijana wake wataingia uwanjani kwa lengo la kupambana  bila kuangalia ama kujali majina na historia ya soka iliyonayo, nchi hiyo.

Kocha Poulsen ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano  na wandishi wa habari hapo jana Jijini Dare es salaam.

Poulsen amesema kuwa haiogopi Ivory Cost isipokuwa anaiheshimu timu hiyo kutokana na kuwa ni miongoni mwa timu bora za soka barani Afrika  ila ana imani kubwa na kikoisi chake kutokana na wachezaji wake kuendelea kubadilika siku hadi siku na kuonesha viwango vizuri vya uchezaji  hivyo wanaingia uwanjani wakitunisha vifua ili kuwakabili bara bara tembo hao wa Ivory Cost na ikiwezekana kuwachakaza.

Katika mkutano huo pia, Poulsen alitumia kuwatoa wasiwasi watanzania kuhusu mbadala wa mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngasa, ambaye hatatinga dimbani katika mechi hii muhimu kwa Tanzania, upon a kwamba hakuna tatizo, ingawa hakutaka kuweka hadharani ni mchezaji gani atakayesimama badala ya Mrisho kwasababu alizoziita za ufundi katika soka.

Mrisho Khalfan Ngasa, hatacheza mchezo huo kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Wakati huohuo, shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, limewataka watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia Stars ili kuweza kuwapa moyo na nguvu wachezaji.
Kisima cha habari kinaitakia kila la heri Stars. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki stars katika mchezo huo

SAFARI YA KUELEKEA BRAZIL KOMBE LA DUNIA

                                        
NI PATASHIKA NGUO KUCHANIKA  UWANJA WA TAIFA 
·  Stars uso kwa uso na Ivory cost.
  Na. Deo Kaji Makomba.  

Patashika nguo kuchina nyasi kuwaka moto inatarajiwa kuanza  majira ya saa tisa alasiri, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dare es salaam.

Patashika hiyo itazihusisha timu za soka za mataifa ya Tanzania na Ivory Cost, ikiwa ni mpambano  katika harakati zile za kuwania kucheza fainali za kombe la dunia hapo mwakani huko nchini Brazil.

Tayari homa ya pambano hilo imekwishakupanda miongoni mwa wachezaji wa timu zote hasa kutokana na umuhimu wa mchezo huo katika hatua hii ya lala salama ya kuwania kuelekea kule Brazil kunako michuano hiyo mikubwa duniani ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne na kuandaliwa na nchi ambayo inakuwa imeshinda ,katika kura ya nchi gani inayositahili kuandaa mashindano hayo, kulingana na shirikisho la soka duniani, FIFA.

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inateremka uwanjani hii leo huku ikiwa na nia moja tu ya kutaka kushinda mchezo huo ili kuweza kujijengea mazingira mazuri ya safari kuelekea Brazil na hivyo kuzidi kuwaongezea raha watanzania walio na kiu kubwa ya muda mrefu kuona Tanzania inabisha hodi katika medani ya soka duniani.

Endapo kama Tanzania itashinda mchezo wake huu dhidi ya Ivory Cost, itakuwa imejikusanyia pointi tisa na hivyo kuongeza matumaini ya safari ya Brazil, wakati Ivory cost ikiishinda Tanzania katika mchezo huu itakuwa tayari na pointi kumi na tatu na hivyo kujihakikishia kukwea pipa kuelekea Brazil hapo mwakani.

Kutokana na kila timu kuuchukulia mchezo huu katika umuhimu mkubwa na wa aina yake hapana shaka itakuwa ni mchezo wa patashika nguo kuchanika nyasi kuwaka moto pale, filimbi ya kwanza ikipulizwa kuashiria kuanza kwa mchakato huo wa lala salama wa kuelekea Brazil hapo mwakani kwa nchi za Afrika.