Thursday 31 October 2013

FUJO ZATOKEA UWANJA WA TAIFA. POLISI WATUMIA MABOMU YA MACHOZI




Polisi wa kutuliza ghasia wakifyatua mabomu ya machozi kutuliza fujo uwanja wa taifa hapo jana, wakati Simba ikicheza na Kagera suger katika mechi ya Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara

Bao la kusawazisha la Kagera Suger katika dakika za lala salama lawachefua mashabiki wa Simba.
·    Baadhi yao wajawa na jazba na kung’oa  viti na kuanza kuvirusha hovyo.
·    Polisi wa kutuliza ghasia watumia mabomu ya machozi kutuliza fujo .
·    Wadau wa soka waeleza hisia zao kutokana na tukio hilo.
·         Wasema si kitendo cha uanamichezo.
                                
                                                   Na. Mwandishi wetu.

Kitendo cha mashabiki wa  timu ya soka ya Simba ya jijini Dar e salaam kufanya fujo na  kung’oa baadhi ya  viti vya uwanja wa Taifa na kuanza kuvirusha  hovyo kimepokelewa kwa hisia tofauti na wapenzi na mashabiki wa soka nchini Tanzania huku wakieleza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mashabiki hao ni utovu wa nidhamu na wanapaswa kuchukuliwa hatua.

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na kisima hiki cha habari alhamis hii mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya timu ya Simba na Kagewra suger wa ligi kuu soka ya Vodacom Tanzania bara, wapenzi na mashabiki hao  wa soka wamesema kuwa si kitendo cha kiungwana watu wakiangalia burudani halafu kikundi Fulani cha watu kuanzisha fujo na hivyo kuharibu burudani.
 Mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba aliyeonekana akifanya fujo hapo akidhibitiwa na polisi wa kutuliza ghasia.

Baadhi ya mashabiki wa timu ya Simba alhamisi hii walijikuta wakishindwa kutuliza jazba zao, baada kuanza kunyofoa viti ndani ya uwanja wa taifa na kuanza kuvirusha hovyo, kufuatia   timu ya Kagera suger kusawazisha bao, lililopatikana kwa njia ya penait kunako dakika za lala salama hali iliyowajaza jazba wapenzi na mashabiki hao wa Simba kuanzisha vurugu kwa mtizamo wa   kuwa, penait iliyotolewa haikuwa sahihi.

Miongoni mwa wadau wa soka aliyezungumza na Kisima cha habari jijini Mwanza,  ni Isack Victor, ambaye amesema kuwa kitendo walichokifanya mashabiki hao si cha kiungwana.

 Baadhi ya viti vya uwanja wa taifa vilivyong'olewa na mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa timu ya Simba.

Victor ambaye pia ni mchambuzi wa soka jijini Mwanza, amesema alivyouona mchezo kupitia Luninga inavyoonekana mashabiki hao hawakuridhishwa na maamuzi yaliyotolewa  na mwamuzi wa mpambano huo ya kutoa penaiti dakika za lala salama hali iliyowafanya mashabiki hao wahamaki na kujawa hasira na kufanya yaliyotokea.

“ Walitakiwa watulize jazba zao, kwani kitendo walichokifanya wala hakiwezi kubadilisha matokeo.” Alisema Isack na kuongeza kuwa “kitendo hicho si cha kiungwana na kiuanamichezo na kinaweza kuwagharimu watu waliofanya fujo hizo kwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

  Mshambuliaji wa timu ya Kagera suger akijaribu kumtoka mlinzi wa timu ya Simba, ambapo timu hizo zilitoka sare ya 1 - 1, kwenye uwanja wa taifa hapo jana.

Katika mchezo huo ambao Simba wakitoka sare ya goli 1 – 1 na Kagera Suger, polisi wa kutuliza ghasia walilazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatuliza mashabiki hao waliamua kung’oa viti na kuanza kuvirusha hovyo hali iliyozua tahaluki ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.