Wednesday 7 August 2013

SEKESEKE LA USAJILI HUKO BARANI ULAYA.



Luis Suarez awataka Liverpool wamuache aende zake.

·       Asema ni wakati wake wa kuondoka

              ·   Wenger ajiandaa kumsainisha, Liverpool bado watia ngumu

              

            Na. deo kaji makomba

Hatimaye mshambuliaji wa klabu ya soka ya Liverpool ya England, Luis Suarez, ameweka hadhari nia yake ya kutaka kuondoka katika klabu hiyo na kujiunga na klabu iliyo katika mashindano ligi ya mabingwa barani ulaya.

Hatua ya Suarez kuweka hadharani nia hiyo ya kutaka “kuwatema” majogoo hao wa Anfiled, imekuja ikiwa hajaambatana na timu yake ambayo hivi sasa iko katika ziara ya kimechezo ya kimataifa huko nchini Norway kutokana na mchezaji huyo kuwa majeruhi, ikiwa ni mandalizi ya hekaheka za ligi kuu ya soka ya England inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay, mwenye umri wa miaka 26, anatarajia kuwasilisha maombi ya uhamisho kwa uongozi wa Liverpool mwishoni mwa wiki, endapo kama mchakato wake wa kutaka kuondoka ndani ya Liverpool utakuwa bado umetiwa ngumu na klabu hiyo yenye masikani yake huko Anfeld.

Suarez ameyaeleza magazeti ya the Guardian na Daily Telegraph ya Uingereza ya kwamba wekundu hao wa Anfeld walimuahidi kuwa anaweza kuondoka katika klabu hiyo kwenye msimu huu wa kiangazi, kama klabu hiyo ingeshindwa kutinga katika ligi ya mabingwa barani ulaya.

“Niliwapa kwa heshima kila kitu katika msimu uliopita. Sasa ninachohitaji ni Liverpool kuheshimu mkataba.” Alisema Suarez katika mahojiano na magazeti hayo.
 Luis Suarez, mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay ambaye anataka kuitema liverpool na kujiunga na klabu ya Asernal
Kulingana na mahojiano aliyoyafanya Suarez na vyombo vya habari, Suarez alisema. “Mwaka uliopita nilikuwa na nafasi ya kuondoka kuelekea katika klabu kubwa barani ulaya na nilibaki kwa mantiki ya kwamba kama tutashindwa kuingia katika ligi ya mabingwa, msimu ujao nitaruhusiwa kuondoka,”

Na tayari washika bunduki wa London, Asernal the gunners, wameonesha nia ya kumtaka Suarez huku wakitangaza dau la zaidi ya paun milioni 40 kama kishawishi cha kutaka kumnasa mchezaji huyo.
Liverpool, ambayo ilimaliza ikiwa ya saba katika msimamo wa ligi kuu ya soka ya England msimu uliopita, tayari “wameichomolea”ofa hiyo na kusisitiza kuwa licha ya Suarez kumaliza mkataba na timu hiyo haiwalazimishi wao kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay.

Suarez, hakuweza kusafiri na kikosi cha Liverpool katika mechi za mandalizi ya kivumbi cha ligi kuu ya soka ya England, huko nchini Norway kutokana na kuwa na majeruhi ya mguu.

Akiwa na Liverpool, Suarez aliweza kuifungia magoli 30 katika mechi 44 alizocheza katika msimu uliopita.
Tangu ajiunge na Liverpool akitokea Ajax Amsterdam ya Uholanzi mnamo januari 2011 kwa dau la paun milioni 22.7, alikwishafunga mabao 51 katika mechi 96, magoli 49 katika michezo 48 akiwa na Ajax kwenye msimu kabla hajajiunga na Liverpool, akifunga magoli 35 katika mechi 69 akiwa na kikosi cha taifa cha Uruguay.

Wakati hayo yakichomoza, bosi wa timu ya soka ya Asernal, Aserne Wenger amekaa mkao wa kula tayari kabisa kumsainisha mshambuliji huyo wa Liverpool, Luis Suarez, na kukiri kuwa mchakato wa uhamisho wa wachezaji umekuwa mngumu tofauti na kawaida katika msimu huu.