Thursday 19 December 2013

HAYA NDIYO YALIYOZUNGUMZWA WAKATI WA MAZISHI YA MWENYEKITI WA ZAMANI WA CCM MKOANI MWANZA, MAREHEMU CLEMENT MABINA (WEMBE).>>>>>>>>>

Umati wa watu walioshiriki katika ibaada ya mazishi ya diwani wa Kisesa na mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, Clement Mabina (Wembe), katika uwanja wa Red Cross, Kisesa.


Wassira,Magufuri waongoza mamia kumzika Mabina.
·    Mazishi yake yafanyika katika eneo lilipotokea tukio
·    Wana Kisesa watakiwa kusamehana kutokana na tukio hilo.
·    Yaelezwa wote ni marehemu watarajiwa.

Na. Baltazar Mashaka.

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, jana waliwaongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya Mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoa Mwanza, Clement Mabina, ayeuawa kikatili mwishoni mwa wiki iliyipita katika kijiji cha Kanyama,wilaya ya Magu.

Wananchi na wakazi wa Kisesa na wa kutoka maeneo mbalimbali ya nje ya mkoa wa Mwanza, walihudhuria mazishi hayo, yaliyofanyika shambani kwake katika kijiji cha Kanyama, majira ya saa 8:00.

Marehemu Mabina ambaye hadi anakumbwa na mauti alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa, azikwa jana mchana katika kilima cha Kanyama, eneo ambalo kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi, walimuua kwa kumshambulia kwa mawe na mapanga.

Kabla ya mazishi, Ibada ya kumuombea marehemu huyo ilifanyika kwenye uwanja Msalaba Mwekundu (Red Cross) ikiongozwa na Paroko wa Parokia ya Bujora, Padre Fabian Muhoja kabla ya waombolezaji hao kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.

Hotuba za mawazi hao ziliwafanya waombolezaji waangue vicheko vya huzuni walipodai kuwa sote ni ‘marehemu watarajiwa akiwemo Paroko aliyeongoza Ibada hiyo na kuwataka wana Kisesa wasameheane na kutohukumiana kutokana na tukio lililosababisha mauaji ya mabina na mtoto Temeli Malimi.

Hatahivyo baadhi ya waombolezaji akiwemo Mbunge wa jimbo la Magu, Festus Limbu na Mwenyekiti wa CCM mkoani Geita, Joseph Kasheku (Msukuma), walishindwa kujizuia na kujikuta wakifuta machozi na kuangua vilio  hadharani baada ya kuelezea mahusiano yao na marehemu.

Akizungumza katika umati huo, Magufuli alisema maelefu ya waombolezaji waliofurika kumuaga mabina ni ushahidi wa jinsi alivyokuwa mwanafamilia na kiongozi mzuri hivyo wakiondoka hapo wawe wamesameheana.

 “Baba Paroko nakushukuru sana kwa mafundisho yako mazuri, sisi sote ni marehemu watarajiwa kuanzia wewe baba Paroko.Tukiondoka hapa tuondoke tumesameheana na tusihukumu maana nasi tutakuja hukumiwa.” alionya Magufuli huku umati wa waombolezaji ukiangua kicheko

 Waziri Magufuri

Waziri huyo alidai wapo watu wanaojua kuchonganisha maneno juu ya misiba hiyo (wa Temeli na Mabina), wapuuzwe na kila mmoja aziombee familia za marehemu hao, sala za kuwalilia Mungu atazipokea.   

Wasira alisema, hakuna mtu anayejua atakavyo kufa sababu hakizuiliki hivyo wanaoshangilia kifo cha Mabina hawana maana kwani kila mmoja hajui atakufa lini na kifo cha aina gani.

“Baba Paroko nakushukuru kwa wosia mzuri, ukiwambia watu hapa wangapi wanaotaka kwenda Mbinguni, wote watanyoosha mikono lakini ukiwauliza wangapi wako tayari kufa, hakuna hata mmoja.Njia ya kwenda Mbinguni ni kufa, hata wewe hutakubali, tunajua ugumu wa jambo hili.” Alisema Wassira.

Wassira aliwaasa wananchi wa Kisesa na Kanyama kuwa kuendeleza ugomvi na fitina hakuwasaidii,hivyo  wajifunze kutokana na vifo vya Mabina na mtoto Temeli Malemi kwa kumaliza migogoro badala ya kutumia nguvu.

Mbunge wa Jimbo la Misungwi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Charles Kitwanga alisema kutokana na kuwa karibu  na marehemu Mabina na familia yake, alishindwa kuongea chochote zaidi ya kutoa pole wananchi wa Kisesa na familia hiyo.

Awali akiongoza Ibada hiyo iliyoanza saa 4:00 asubuhi, Paroko wa parokia hiyo ya Bujora, Padre Mhoja alisema kukosekana kwa upendo na hofu ya Mungu miongoni mwa wanajamii wa Kisesa na Kanyama ndiyo sababu ya mauaji hayo.

Padre Mhoja aliwafariji waombolezaji na wananchi wa maeneo hayo watakiane amani kwa kupendana na kusameheana.

Pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kutoka mkoani Mwanza na nje ya mkoa huo, wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Balozi Gertrude Mongela na Seleman Kikwete aliyeiwakilisha familia ya Rais Jakaya Kikwete.

 Green gurd wakiwa wamebeba jeneza la kamanda wao marehemu Clement Mabina(Wembe)

Wengine ni wabunge Lameck Airo (Rorya), Andrew Chenge (bariadi Magharibi), wakuu wa mikoa ya Dar es salaam Mecky  Sadiki, Said Magarula (Geita), wakuu wa wilaya za Butiama, Sengerema, Misungwi, Busega, Chato, Magu na viongozi wa Chama wa mkoa huo na jirani.


No comments:

Post a Comment