Thursday 10 October 2013

MAUAJI YA KINYAMA NA YA KUTISHA YATOKEA JIJINI MWANZA





 Mkaguzi  Msaidizi wa Polisi, Bi. Levina mwenye simu ya upepo akiwasiliana na makao makuu ya jeshi hilo kutoka eneo la tukio. Hapa mwili wa marehemu ambaye jina halijafahamika ambaye anatuhumiwa kumwua mwenzake kwa kumchoma kisu ukiwa umelala chini huku mawe yaliyotumika kumwulia yakioneka. Pembeni ni kisu akichokitumia katika mauaji ya kijana mmoja ambaye naye jina halikufahamika.



Mauji ya kinyama na kutisha yatokea Jijini Mwanza.




  •  Ni baada ya mtu mmoja jina halikufahamika  kuanza kumkimbiza na kisha kumchoma kisu.

  •    Naye auwawa kikatili na wananchi wenye hasira kali.

  •      Kisima cha habari chashuhudia tukio hilo.



                        Na. Mashaka Baltazari.

Mtaa wa Sheikh Amin uliko Msikiti wa Ijumaa,katikati ya Jiji la Mwanza, jumatano hii  umegeuka kuwa uwanja wa damu baada ya watu wawili kuuawa katika tukio moja.

Mauaji hayo ya kinyama na ya kikatili kabisa kuwahi kutokea jijini Mwanza, yalitokea majira ya asubuhi kati ya saa 2:45 na 3:00,wakati ambao watu mbalimbali walikuwa wakielekea katika shughuli zao za kila siku na wengine wakisafiri.

Mwandishi wa Kisima cha habari,  alishuhudia baadhi ya watu wakikimbilia eneo la mtaa huo wa Sheikh Amin,ambapo bila ajizi alifanya hima kufahamu nini kimetokea.

Akiwa mita 20 kutoka barabara ya Nyerere,alishuhhudia umati wa watu wamekusanyika jirani na lango la kuingilia msikitini,huku wengine wakizidi kukimbia jirani na zahanati ya Msikiti wa Ijumaa.



 Baadhi ya wananchi wakishuhudia mwili wa marehemu  Abubakar Mudilkati, ukiwa umelala chini katikati ya magari . Marehemu huyo alichomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake jumatano hii majira ya asubuhi na kupoteza maisha papo hapo.


 Baada ya kujongea karibu katika kusanyiko la kwanza alikuta kijana mmoja ambaye jina halikufahamika mara moja, akipumua kwa shida huku damu nyingi zikitoka mdomoni na puani baada ya kupigwa kwa mawe makubwa kichwani na wananchi wenye hasira kali akituhumiwa kumwua Abubakar Mudilkat.

Kipigo hicho cha wananchi, ilisababisha kichwa cha kijana huyo aliyekuwa amevaa suruali ya aina ya jeans kubonyea upande wa kushoto,ambapo chini kulikuwa na kisu chenye mpini wa rangi nyekundu,nyeupe na blue.

Katika mahojiano na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, ambao hawakutaka majina kutajwa,walisema marehemu alikuwa amemwua Abubakar  kwa kumchoma visu sehemu ya kulia shingoni,tumboni katika ubavu wa kushoto na katika bega la kulia .


 Baadhi ya wananchi wakishuhudia mwili wa marehemu wa Abubakar Mudilkati, ukiwa umelala chini katikati ya magari .marehemu huyo alichomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake jana majira ya asubuhi na kupoteza maisha papo hapo.


Walisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye naye ni marehemu kwa sasa,baada ya unyama  huo alijaribu kukimbia lakini wananchi wenye hasira wakamuwahi na kumshushia kipigo kilichosababisha kifo chake papo hapo.

Aidha mashuhuda hao walikaririwa wakisema muuaji huyo kabla ya kumchoma marehemu kwa kisu, alisikika akimtuhumu  kuwa alimwua baba pamoja na mama  yake na bado  anamfuatilia hadi sasa.


 Gari la polisi likiwa limebeba mwili wa marehemu aliyeuawa na wananchi baada ya kumwua mwenzake kwa kumchoma kisu.(Picha zote na Mashaka Baltazar)

"Alikumkuta marehemu Abubakr akiteka maji bombani, akamwambia anachota maji yake yeye atakula wapi. Baadaye akadai hawataki kumpa vyake akala, lakini ipo siku watagombea maiti yake kwenda kuizika,"alisema mmoja wa mashuhuda hao bila kutaka kutajwa jina.

shuhuda huyo alisema baada ya hapo alimgeuzia kibao marehemu Abubakar akituhumu kuwa aliwauwa wazazi wake ndipo akanza kumfukuza kabla ya kumchoma kisu.

Ilielezwa kuwa  marehemu Abubakar alikuwa akifanya kazi kwa mama ntilie  aliyetajwa kwa jina moja la Sifa na alikuwa na siku nne tu tangu atoke kwao Bukoba mkoani Kagera, kuja jijini  Mwanza kutafuta kazi.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, DCP Ernest Mangu alipoulizwa kuhusiana na tukio la mauaji ya watu hao, alidai hana taarifa na kuahidi kumtuma Mkuu wa Upelelezi neo la tukio.

“Watu wawili wameuawa hapo msikiti wa Ijumaa asubuhi ya jumatano hii ! Mbona taarifa sina,hebu ngoja nimtume RCO aje hapo,”alisema DCP Mangu kwa simu.

Hata hivyo muda mfupi  Polisi Wilaya ya Nyamagana waliwasili eneo la tukio wakiongozwa na Mkaguzi wa jeshi hilo,WP Levina kwa ajili ya kuchukua maelezo kwa mashuhuda na miili ya marehemu hao .

UWEKEZAJI WA ELIMU KWA KIZAZI CHA TANZANIA

Pichani Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa,Meshach Bandawe kushoto, akikabidhi sehemu ya vitabu vya kiada na ziada Mkuu wa shule ya Sekondari Mwamanga, Oscar Deogratius .Wa kwanza kushoto ni watumishi was PPF na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo. (Picha na Mashaka Baltazar.)

Katika kutambua umuhimu wa elimu kama urithi mkubwa kwa kizazi cha Tanzania.

 

  • ·        Shirika la mfuko wa hifadhi ya Jamii, PPF, latoa vifaa mbalimbali  vya masomo

  •  Shule ya sekondari ya Mwamanga wilayani Magu yanufaika na msaada huo.


                        

                                Na.Mashaka Bartazal.




MFUKO wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, umetoa msaada wa vitabu vya masomo mbalimbali,kwa shule ya Sekondari  Mwamanga,Katani humo Wilaya ya Magu,Mwanza.

Vitabu hivyo vyenye thamani ya sh.2 milioni,vilikabidhiwa jana kwa Mkuu wa shule hiyo, Oscar Deogratius na Meneja wa Mfuko wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshach Bandawe na kushuhudiwa na baadhi ya walimu, wanafunzi na watumishi wa mfuko huo.

Bandawe alisema, vitabu hivyo vitasaidia kukuza uelewa wa wanafunzi hasa wa masomo ya sayansi ambayo kwa kipindi kirefu sasa, baadhi ya wanafunzi wanakwepa kuyasoma kwa sababu ya ukosefu wa vitabu vya masomo hayo.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu kuwa  urithi pekee kwa vizazi vyetu,mfuko umekuwa ukisaidiana na serikali kutatua changamoto za elimu, kuhakikisha kizazi cha sasa kinanufaika na huduma zinazotolewa na PPF.

“PPF tunaongozwa na sera, kushiriki masuala ya kijamii katika sekta ya afya na elimu.Pamoja na kulipa mafao ya wanachama wetu,fao la elimu na ujenzi wa Vyuo Vikuu kama Dodoma na Nelson Mandela cha Arusha, wanaofaidika ni watoto wa wanachama wetu na wasio wa wanachama.Ni wajibu wetu kuisaidia serikali kuhakikisha taifa linakuwa na vijana walioelimika,”alisema Bandawe.

Picha ikionesha moja ya jengo la kitega uchumi la mfuko wa hifadhi ya jamii, PPF, katikati ya jiji la Mwanza.Jengo hilo limesheheni maofisi mbalimbali pamoja na hotel ya hadhi ya nyota tano(Five star) Gold Crest hotel(Picha na maktaba ya Kisima cha habari)


Alisema watoto hao wakipata elimu na kuingia kwenye soko la ajira, watasaidia kukuza uchumi wetu ikiwa ni pamoja na kujiunga na mfuko huu na kuufanya uwe endelevu kwa vizazi vijavyo.

Msaada huo wa vitabu unahusisha masomo ya Hisabati, Kemia, Bailolojia,Jiografia,Fizikia, Kiswahili, Kiingereza na Uraia vyote vikiwa vya mtaala mpya.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ya sekondari Mwamanga,Deogratius, alisema msaada huo wa vitabu umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wanafunzi sita kuchangia kitabu kimoja.

Alisema vitabu hivyo vitaamsha  ari na morali ya wanafunzi kujifunza, tofauti na hapo awali na kuahidi watavitumia vizuri kufundisha na kujifunzia  wanafunzi ili kuwajenga vizuri kitaaluma, hatimaye waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Aidha akitoa shukurani kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, mwanafunzi wa kidato cha tatu, Philipo Bukesi aliupongeza mfuko wa PPF kwa  msaada huo na kuomba mashirika na makampuni mengne kuiga mfano huo,katika kuboresha elimu nchini na sasa kitabu kimoja kitatumiwa na wanafunzi wawili badala ya sita.

Mwingne ni Veronica Sylvester waa kidato cha tatu pia,alisema walikuwa wakipata shida ya kujifunza masomo ya sayansi  na kuazimika kusoma kwa makundi kutookana na uhaba wa vitabu,lakini sasa hali hiyo itapungua.Shule hiyo ina wanafunzi 514.