Thursday 15 August 2013

Kamanda wa polisi mkoani mwanza, Bwana Ernest Mangu, akizungumza na Kisima cha habari ofisini kwake jijini Mwanza.(Picha na Deo Kaji Makomba)


Baada ya  polisi kupambana na  kuyaua majambazi matatu yaliyokuwa na silaha jijini Mwanza;

  • Safari hii yakamata meno ya tembo.
  • Yalikuwa yamefungwa kwenye gunia la mkaa ili “kuwazuga”      polisi.



                                 Na. deo kaji makomba

Katika kuhakikisha linafanya kweli kwenye harakati zake za kupambana na matukio ya kiarifu, jeshi la polisi mkoani Mwanza, limekamata nyara za serikali zilizokuwa zikisafirishwa kutoka mkoani Mara na hatimaye kukamatwa jijini Mwanza.

Nyara hizo za serikali ni meno ya tembo ambayo yalikamatwa na asikari polisi waliokuwa katika doria jumatano hii katika kituo kikuu cha mabasi cha Buzuruga jijini Mwanza.

Tukio hilo la kukamatwa kwa nyara hizo za serikali jijini Mwanza jumatano hii, limetokea siku chache tu, mara baada ya jeshi hilo la polisi mkoani Mwanza kupambana kwa kufyatuliana risasi na majambazi yaliyokuwa na silaha aina ya sub machine gun (SMG) yakiwa katika harakati za kutaka kupora na kufanikiwa kuyauwa.

Akizungumza na kisima cha habari jijini Mwanza, kamanda wa polisi mkoani humo Bwana Erenest Mangu, amesema kuwa, tukio la kukamatwa kwa meno hayo ya tembo, lilitokea majira ya saa tatu na robo asubuhi.

Kulingana na kamanda Mangu, mnamo majira hayo ya saa tatu asubuhi, alikamatwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Yohana Jackson Charles (27) mkazi wa Butiama mkoani Mara, akiwa na vipande kumi vya meno ya tembo.

Kamanda Mangu ameongeza kuwa meno hayo ya tembo yalipopimwa uzito wake umefikia  kilo 26, yakiwa na thamani ya shilingi milioni ishirini na tatu laki mbili.

Meno hayo ya tembo yalikuwa yamefungwa kwenye junia la mkaa ili “kuwazuga” kama si kuwahadaa watu wa usalama kama anavyoelezea kamanda Mangu wakati akizungumza na Kisima cha habari ofisini kwake jijini Mwanza.