Monday 18 November 2013

CHUPA 40,000 ZA DAMU ZATAKIWA KANDA YA ZIWA.

Mmoja wa watu akijitolea damu kwa ajili ya kuchangia benki ya damu kusaidia watu wanaokuwa na mahitaji ya huduma wakati wanapokuwa wamepungukiwa damu.

Chupa 40,000 za damu zahitajika.
·    Ni katika kituo cha taifa cha mpango wa damu salama kanda ya ziwa.
·    Lengo ni kukabiliana na upungufu wa damu katika hospitali kanda ya ziwa.

                   Na. Mashaka Bartazal.

KITUO cha Taifa cha Mpango wa Damu Salama, Kanda ya Ziwa, kinahitaji chupa 40,000  za damu ili kukabiliana na upungufu wa damu kuweza kuhudumia hospitali za mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Upungufu huo ulibainishwa jana Jijini  Mwanza na Ofisa Mhamasishaji wa Mpango wa Damu Salama Kanda ya Ziwa, Vincent Muhada, akizungumza wakati wa zoezi la uchangiaji damu salama kwa hiari, lililoandaliwa na Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania.

Alisema, mahitaji halisi ya damu salama kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ni chupa 70,000, lakini hadi sasa chupa zinazopatikana ni kati ya  25,000 hadi 30,000 , hivyo kuwa na upungufu wa chupa 40,000.

Muhada, tatizo la upungufu wa damu salama linasababishwa na jamii yenyewe kutoshiriki kikamilifu kujitolea kwa hiari kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo hospitalini.

Alisema  Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania inastajhili kupongezwa kutokana na moyo wa kujitolea kuchangia damu salama,kwani hali  itasaidia jamii na wagonjwa waliolazwa hospitalini kupata mahitaji ya damu.

“Niipongeze taasisi hihi kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine wenye mahitaji ya damu.Mahitajii halisi ya damu, ni chupa 70,000 kwa mwaka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Lakini hadi sasa tuna chupa 25,000 hadi 30,000 tu! Tatizo laupungufu huo linatokana na  wananchi kuogopa kujitolea kuchangia damu,” Muhada.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Bilal Muslim Mission of Tanzania, Sibtain Meghji, aliitaka jamii kujitolea kwa moyo mmoja kuchangia damu, kwani hiyo itasaidia sana kuokoa wagonjwa wenye kuhitaji damu waliopo hospitalini na wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Alisema kila mwaka taasisi hiyo  kwa kushirikiana na waumini wote wa madhehebu ya Shia Ithna Asheri, wamekuwa wakiendesha mpango huo wa kuchangia damu, na zoezi hilo jana lilitarajiwa kukusanya zaidi ya chupa 400 kutokana na idadi ya watu waliojitokeza.

“Taasisi yetu imekuwa mstari wa mbele  kuhamasisha waumini wa dini ya madhehebu ya Shia  na jamii kujitolea kuchangia damu kwa ajili ya watu wenye matatizo.,” alisisitiza Meghji.

Aidha, Meghji aliviomba vyombo vya dola kutekeleza vema majukumu yake kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaohujumu kwa kuuza damu hospitalini, na kuiomba jamii kujitokeza kwa wingi kuchangia damu punde zoezi hilo linapofanyika.

Mmoja wa watu wa kwanza waliojitolea kutoa damu katika zoezi hilo, Hussein Shaban, aliwaambia waandishi wa habari kwamba: “Kila mwaka mimi lazima nitoe damu kwa ajili ya binadamu wenzangu wanaohitaji damu hospitalini. Na naomba sana watu wengine wajitolee ili tuokoe maisha ya ndugu zetu, maana binadamu wote ni sawa”.

Kituo cha Taifa cha Damu Salama Kaya Ziwa kinahudumia hospitali zote za mikoa ya Mwanza,Mara,Kagera,Shinyanga,Geita,Tabora na Kigoma