Tuesday 31 December 2013

TASAJA YAJITOSA MGOMO WA WAFANYABIASHARA MWANZA.>>>>

Afisa habari wa TASAJA, Bituro Kazeri aliyenyoosha mikono wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Mwanza.

TASAJA yajitosa mgomo wa wafanyabiashara Mwanza.
·    Yawataka wafanyabiashara warudi kutoa huduma kwa jamii.
·    Yasema hoja waliyonayo wafanyabiashara ni ya msingi, lakini njia waliyoitumia sio sahihi.

Na. Baltazar Mashaka.

TAASISI  Sayansi ya Jamii (TASAJA) ya Jijini Mwanza, imeingilia kati mgomo wa wafanyabiashara ikitaka watafakari na kusitisha mgomo huo, kwa madai kuwa hauna tija kwa maslahi ya nchi na jamii.

TASAJA pia   imewataka warudi kutoa huduma kwa jamii na serikali ibebe mzigo wa kusambaza mashine hizo kielektroniki ,Electronic  Fiscal Device (EFD) kwani haitapoteza chcochote, ili kuondokana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mgomo huo.

Afisa habari wa TASAJA, Bituro Kazeri, akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Mwanza,  alisema hoja ya wafanyabiashara hao  kuhusu gharama kubwa za kununulia mashine za Ankara za kutolea kodi ni ya msingi, lakini njia waliyotumia ya mgomo, si njia sahihi ya kutatua  matatizo bali ni kufungua mlango mwingine wa  matatizo.

“Wafanyabiashara kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakinung’unika  kupinga matumizi ya  mashine  maalum za Ankara za  kutolea kodi (EFD ) wanapouza bidhaa zao. Ununuzi wa  mashine hizo umezua  migomo na kuathiri huduma za kijamii na kiuchumi na kwa siku hizo ya serikali haikuingiza mapato.

Mgomo huo utakuwa na madhara makubwa kwa jamii siku za karibuni,kama mishahara, ukosefu madawa  hospitali na huduma zingine za msingi ”alisema Kazeri.

Alisema serikali pekee ikiachiwa mzigo huo wa kuagiza mashine hizo lazima gharama kubwa zitarudi kwa walaji na ni kuwabebesha mzigo mkubwa  wa kodi. Lakini pia watumiaji wakiachiwa wazinunue kinachogomba ni upatikanaji wake. 

“Sidhani  kama tutafikia hatua mashine  hazitatumika, na matokeo tunayotaka kwa njia ya mgomo hayataondoa hilo. Ndiyo maana TASAJA tunaitaka serikali irudi kule inakokopa ,ikiwezekana izungumze na benki ya dunia watukopeshe tununue mashine hizo tutalipa,”alisema Kazeri.

Aidha alisema wao TASAJA wanaunga mkono hoja za Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa matumizi ya mashine hizo yanalenga kupunguza mianya ukwepaji kodi na mianya ya rushwa miongoni mwa wakusanya kodi wasio waaminifu, kuongeza na kuboeresha ukusanyaji kodi na utunzaji kumbukumbu za mauzo na manunuzi .

Kazeri alidai kuwa teknolojia hiyo ya kutumia mashine za kutolea Ankara za kodi ikitumika vizuri, itaboresha ukusanyaji  kodi  na kuweka kumbukumbu sahihi zinazotiliwa shaka na maofisa wa kodi . Kwamba njia hiyo ndiyo inayotumika duniani kote na itaondoa manung’uniko na lawama kati ya wafanyabiashara na watoza kodi.

“Mfumo huu ukiangaliwa kisayansi litakuwa ni jambo bora,Tunachokata ni upatikanaji wake.Ukinunua serikali itakulipa kupitia kodi unayopaswa kuilipa.Hii ni faida kwa serikali,wafanyabiashara na lazima watumiaji wafahamu faida zake na elimu ya matumizi ya mashine hizo za Ankara za kutolea kodi,”alifafanua Kazeri.

Alisema kuwa miradi mingi ya kuboresha ukusanyaji wa mapato nchini imekuwa ikipatya ufadhili wa Benki ya Dunia, hivyo ni vema Serikali ikaangalia uwezekano wa kufanya nayo mazungumzo au wahisani wengine ipate fedha za kununulia mashine hizo ni kuzigawa bila kujali ukubwa wa biashara.

Alisema matumizi ya mashine hizo kwa kiwango kikubwa yataiwezesha nchi kuongeza ukusanyaji kodi,kujenga na kukuza utamaduni wa kuchukua Ankara za mauzo na manunuzi ,ambao kwa hapa nchini ni wa kiwango cha chini na utajenga uhusiano mzuri baina ya wadau wa kodi ambao ni serikali,wafanyabiashara,watoza kodi na jamii.

“Kodi ndiyo uhai wa serikali na ustawi wa wananchi wake.Hakuna njia nyingine ya serikali kupata kodi mbalimbali bila kuwatoza wananchi wake kwa njia sahihi na uwazi mkubwa.TASAJA tunapendekeza matumizi ya mashine za kutolea Ankara ni njia muafaka ya kuleta ukusanyaji  kodi sahihi na wa haki .Kila mdau anapaswa kuliunga mkono zoezi hili,”alisema Kazeri.

Wafanyabiashara wamekuwa wakituhumiwa kutumia vitabu viwili vya Ankara za kodi ,kutiliwa shaka kwa kumbukumbu zao  za biashara na maofisa wa kodi  hali ambayo imekuwa ikisababisha wakadiriwe kodi siyosahihi.

Kwamba TRA nao wanatuhumiwa kuwapandishia kodi wafanyabiashara katika makadirio ya kodi. Makadirio hayo makubwa yalikuwa yakijenga mazingira na njia ya kushawishi na kulazimisha rushwa,mambo yanayopingwa na wafanyabiashara.

Hata hivyo Kazeri alisema ujio wa mashine za kutolea Ankara za kodi ndiyo jibu muafaka la matatizo yanayouzingira mfumo wa ukusanyaji kodi na uhusiano kati ya wafanyabiashara na watoza kodi na ni njia ya kisayansi ya kushughulikia suala hilo.