Sunday 29 December 2013

RAGE BADO NI MWENYEKITI HALALI WA SIMBA.>>>>>>>>>

Mwenyekiti halali wa Klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba, Ismail Aden Rage.


Rage ndiye mwenyekiti halali wa Simba.
·    Maamuzi yaliyochukuliwa na kamatia ya utendaji ya Simba kumsimamisha yaelezwa ni batili.
·    Agizo la TFF kumtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa wanachama bado lipo palepale.
·    Nalo sakata la Okwi, TFF ladai kulitambua.

Na. Deo Kaji Makomba.

Ismail Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.

Kauli hiyo ya Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inakuja kufuatia kubaini  mapungufu kadhaa ya kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao, katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jumamosi iliyopita jijini Dar es salaam.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, na kusambazwa na ofisa habari wa Shirikisho hilo, Boniface Mgoyo Wambura na kasha nakala yake kukifikia Kisima cha habari, imebainisha  Upungufu huo kuwa  ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.

Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.

Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale.

Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.

Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.

TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.

Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.

Ama kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.

Wakati huo huo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.

Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.

Baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.

Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.

Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.

MOURINHO AITABILIA LIVERPOOL UBINGWA WA LIGI KUU YA ENGLAND.>>>>>>>>>>>

Kocha wa timu ya soka ya Chelsea Jose Mourinho.


Mourinho aitabiria Liverpool kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya England.

Na. Deo Kaji Makomba.

Kocha mkuu wa Chelsea Jose Mourinho anaamini kuwa klabu ya Liverpool ndiye bingwa wa ligi kuu ya England kwa msimu huu kwani kwa sasa Kocha wa timu hiyo Brendan Rodgers atakuwa na kazi moja ambayo ni kuangazia ligi hiyo.

Mourinho anahisi Liverpool kutoshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya itawasaidia kunyakua kombe hilo walilolikosa kwa miaka 24 iliyopita.

"Hawashiriki kwenye joto la mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya wala ya Europa league Mourinho," amesema.

"Ubora wa timu pamoja na ari hiyo ndio faida yao ni kweli wanaweza kushinda kombe".
Timu za Chelsea, Manchester United, Manchester City na Arsenal wanashiriki mashindano ya Klabu Bingwa barani Ulaya ambapo Mourinho anaamini kwamba Liverpool watamalizia mechi chache kama 20 tofauti na washindani wao kwa msimu huu.

"Hawa wachezaji watacheza mechi zipatazo 60. Liverpool itacheza mechi 40. Hii ni tofauti kubwa sana," aliendelea.

"Liverpool watakuwa kwenye mapumziko kwa msimu mmoja, wiki moja ya kujiandaa kwa mechi, watacheza mechi, wiki moja watajiandaa kwa mechi inayofuata. Hii ina faida, ni manufaa yasiyodhaniwa."

MAKAMBA AWEZESHA MKOPO KWA WAENDESHA BODA BODA 1,745 MWANZA.>>>>>>

 Naibu waziri wa mawasiliano, Sayansi na teknolojia, January Makamba.


Makamba awezesha mkopo kwa waendesha Bodaboda 1,745 Mwanza.
·    100 awalipia bima ya maisha.
·    Asema kuendesha pikipiki za kusafirishia abiria ni kazi salama.


Na. Baltazar Mashaka.


NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,January Makamba,amewezesha waendesha pikipiki 1,745 kati ya 4861 waliopo mkoani Mwanza, kukopeshwa pikipiki kwa bei nafuu ili kuwakwamua na umasikini wa kipato.

Mbali na mkopo huo wa pikipiki hizo aina ya FECON kutoka kampuni ya Tanzania China Dev ltd ya nchini China,Makamba pia aliwalipia bima ya maisha waendesha pikipiki 100 walioshinda bahati nasibu iliyoendeshwa kwenye uwanja wa Nyamagna Jijini Mwanza.

Akizungumza kwenye kongamano hilo la siku moja la waendesha pikipiki hao,Makamba alisema uwezeshaji huo wa pikipiki, ameufanya kwa nia njema na upendo kwa vijana hao  ili wajiajiri badala ya kuajiriwa na hatimaye waajiri vijana wenzao.

Alisema kuendesha pikipiki za kusafirisha abiria ni kazi salama na si sahihi ikachukuliwa kama leseni ya vifo na ulemavu  kwa madereva na abiria wao,hivyo akawataka waone umuhimu wa kujiunga na bima ya maisha itakayowakinga wanapopata ajali badala ya kukata bima za vyombo pekee na kuacha maisha ya madereva yakiwa hatarini.

“Wapo wapo wanauliza kwa nini niko hapa,na kwa nini asiwe mtu mwingine na ni vipi nilete shughuli zangu hapa.  Nashukurru mwenyekiti wenu amelizungumza vizuri suala hili. Alnifuata kuomba niwasaidie mpate pikipiki zenu wenyewe kwa sababu nyote hapa mnaendesha za watu wengine,” alisema Makamba na kuongeza;

“Sipo hapa kwa ajili ya urais na si sababu ni msimu wa siasa, la hasha. Lakini wapo watu wengine wanatumia boda boda (pikipiki) kufanya siasa. Sisi tulianza kimya kimya muda mrefu ili kujikomboa na umasikini wa kipato.Je, wao walikuwa wanafahamu ? Zimetengwa pikipiki 1,745 za kuwakopesheni vijana  wenzangu kila mmoja amiliki ya  kwake na baaadaye muweze kuajiri wengine.”

Makamba alisema zaidi kuwa; “Watu wengine wanaohoji kwa nini niko hapa ,watakapokuja kufikiria hilo tayari watakuta sisi tumeanza na tumepiga hatua ingawa sifanyi haya kwa dhamira ya urais kama wanavyodai watu wengine, bali upendo nilio nao wa kusaidia vijana wenzangu kupambana na changamoto za ukosefu wa ajira na maisha .”  

Alifafanua kuwa pikipiki hizo 1,745 ni mkopo wa bei nafuu kutoka kampuni ya Tanzania China Dev ltd baada ya kuomba ambapo thamani yake ni shilingi 2,879,250,000 na zitatolewa kwa awamu tatu na tayari awamu ya kwanza zimetolewa pikipiki 265.Awamu ya pili zitatolewa 450 na ya tatu pikipiki 1000.


“Sasa nataka mambo haya yafanyike waliokopeshwa warejeshe mapema ili wengine nao wanufaike kwa kukopa pia pikipiki hizo.

Lakini  kazi ya pikipiki isiwe leseni ya vifo na ulemavu kwa watu,hilo hatulitaki. Zingateni sheria, sababu kulikuwa na mjadala serikalini kuruhusu ama kutoruhusu usafiri wa pikipiki. Kwa kuwa usafiri wa mabasi haukukidhi ndiyo maana ukaruhusiwa,”alisema Makamba.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo alisema ajali za pikipiki zimeongezeka kwa kasi na kusababisha ulemavu na vifo,hivyo ipo haja ya kuzipunguza ajali hizokwa kutii sheria na kutoa elimu ya kutosha kwa waendesha pikipiki na kuwahamasisha kujiunga na makampuni na mashirika ya bima ili kujikinga na ajali hizo.

Makamba alidai takwimu za ajali za pikipiki za mwaka 2001 zinaonyesha watu 965 walipoteza maisha huku mwaka 2012 ajali hizo zikisababisha vifo vya watu 930, hali inayoonesha watu wengi watapoteza maisha yao kwa ajali za pikipiki kuliko UKMWI na kusisitiza waendesha pikipiki kuzingatia na kufuata na kutii sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndiklo,aliwataka waendesha pikipiki wa mkoani hapa,kutambua kuwa kazi ya kusafirisha abiria ni shughuli halali ya kuwaingizia kipato na kuengeneza maisha yao.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa usafiri huo wa pikipiki, serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, huku akiwataka madereva kupata elimu ya matumizi sahihi ya barabara ili kazi yao ifanyike kwa amani na usalama .

Mbali na Mkuu wa mkoa  Ndikilo na  Makamba ambaye alikubali kuwa mlezi wa Umoja wa Waendesha Pikipiki mkoa wa Mwanza (UWP),  kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula,Diwani wa Nyamagana, Bhiku Kotecha pamoja na wadau mbalilmbali wa usafiri.