Sunday 29 December 2013

MAKAMBA AWEZESHA MKOPO KWA WAENDESHA BODA BODA 1,745 MWANZA.>>>>>>

 Naibu waziri wa mawasiliano, Sayansi na teknolojia, January Makamba.


Makamba awezesha mkopo kwa waendesha Bodaboda 1,745 Mwanza.
·    100 awalipia bima ya maisha.
·    Asema kuendesha pikipiki za kusafirishia abiria ni kazi salama.


Na. Baltazar Mashaka.


NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,January Makamba,amewezesha waendesha pikipiki 1,745 kati ya 4861 waliopo mkoani Mwanza, kukopeshwa pikipiki kwa bei nafuu ili kuwakwamua na umasikini wa kipato.

Mbali na mkopo huo wa pikipiki hizo aina ya FECON kutoka kampuni ya Tanzania China Dev ltd ya nchini China,Makamba pia aliwalipia bima ya maisha waendesha pikipiki 100 walioshinda bahati nasibu iliyoendeshwa kwenye uwanja wa Nyamagna Jijini Mwanza.

Akizungumza kwenye kongamano hilo la siku moja la waendesha pikipiki hao,Makamba alisema uwezeshaji huo wa pikipiki, ameufanya kwa nia njema na upendo kwa vijana hao  ili wajiajiri badala ya kuajiriwa na hatimaye waajiri vijana wenzao.

Alisema kuendesha pikipiki za kusafirisha abiria ni kazi salama na si sahihi ikachukuliwa kama leseni ya vifo na ulemavu  kwa madereva na abiria wao,hivyo akawataka waone umuhimu wa kujiunga na bima ya maisha itakayowakinga wanapopata ajali badala ya kukata bima za vyombo pekee na kuacha maisha ya madereva yakiwa hatarini.

“Wapo wapo wanauliza kwa nini niko hapa,na kwa nini asiwe mtu mwingine na ni vipi nilete shughuli zangu hapa.  Nashukurru mwenyekiti wenu amelizungumza vizuri suala hili. Alnifuata kuomba niwasaidie mpate pikipiki zenu wenyewe kwa sababu nyote hapa mnaendesha za watu wengine,” alisema Makamba na kuongeza;

“Sipo hapa kwa ajili ya urais na si sababu ni msimu wa siasa, la hasha. Lakini wapo watu wengine wanatumia boda boda (pikipiki) kufanya siasa. Sisi tulianza kimya kimya muda mrefu ili kujikomboa na umasikini wa kipato.Je, wao walikuwa wanafahamu ? Zimetengwa pikipiki 1,745 za kuwakopesheni vijana  wenzangu kila mmoja amiliki ya  kwake na baaadaye muweze kuajiri wengine.”

Makamba alisema zaidi kuwa; “Watu wengine wanaohoji kwa nini niko hapa ,watakapokuja kufikiria hilo tayari watakuta sisi tumeanza na tumepiga hatua ingawa sifanyi haya kwa dhamira ya urais kama wanavyodai watu wengine, bali upendo nilio nao wa kusaidia vijana wenzangu kupambana na changamoto za ukosefu wa ajira na maisha .”  

Alifafanua kuwa pikipiki hizo 1,745 ni mkopo wa bei nafuu kutoka kampuni ya Tanzania China Dev ltd baada ya kuomba ambapo thamani yake ni shilingi 2,879,250,000 na zitatolewa kwa awamu tatu na tayari awamu ya kwanza zimetolewa pikipiki 265.Awamu ya pili zitatolewa 450 na ya tatu pikipiki 1000.


“Sasa nataka mambo haya yafanyike waliokopeshwa warejeshe mapema ili wengine nao wanufaike kwa kukopa pia pikipiki hizo.

Lakini  kazi ya pikipiki isiwe leseni ya vifo na ulemavu kwa watu,hilo hatulitaki. Zingateni sheria, sababu kulikuwa na mjadala serikalini kuruhusu ama kutoruhusu usafiri wa pikipiki. Kwa kuwa usafiri wa mabasi haukukidhi ndiyo maana ukaruhusiwa,”alisema Makamba.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo alisema ajali za pikipiki zimeongezeka kwa kasi na kusababisha ulemavu na vifo,hivyo ipo haja ya kuzipunguza ajali hizokwa kutii sheria na kutoa elimu ya kutosha kwa waendesha pikipiki na kuwahamasisha kujiunga na makampuni na mashirika ya bima ili kujikinga na ajali hizo.

Makamba alidai takwimu za ajali za pikipiki za mwaka 2001 zinaonyesha watu 965 walipoteza maisha huku mwaka 2012 ajali hizo zikisababisha vifo vya watu 930, hali inayoonesha watu wengi watapoteza maisha yao kwa ajali za pikipiki kuliko UKMWI na kusisitiza waendesha pikipiki kuzingatia na kufuata na kutii sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndiklo,aliwataka waendesha pikipiki wa mkoani hapa,kutambua kuwa kazi ya kusafirisha abiria ni shughuli halali ya kuwaingizia kipato na kuengeneza maisha yao.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa usafiri huo wa pikipiki, serikali itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, huku akiwataka madereva kupata elimu ya matumizi sahihi ya barabara ili kazi yao ifanyike kwa amani na usalama .

Mbali na Mkuu wa mkoa  Ndikilo na  Makamba ambaye alikubali kuwa mlezi wa Umoja wa Waendesha Pikipiki mkoa wa Mwanza (UWP),  kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula,Diwani wa Nyamagana, Bhiku Kotecha pamoja na wadau mbalilmbali wa usafiri.

No comments:

Post a Comment