Monday 17 June 2013

LICHA KUFUNGWA 4-2 NA IVORY COST, HARAKATI ZA KWENDA BRAZIL


·         Watanzania wasema wana matumaini na Stars ya sasa kufanya vyema siku za usoni.
·         Wataka kutiliwa mkazo kwa soka la vijana na kwamba lolote linawezekana.

         

Na. Deo Kaji Makomba

Licha ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa stars, kufungwa mabao 4-2 na timu ya soka ya taifa ya Ivory Cost katika mechi ya harakati ya kuwania kuelekea katika fainali za kombe la dunia  huko nhini Brazil hapo mwakani, wapenzi na mashabiki wa soka nchini Tanzania, wamelezwa kuridhishwa na kiwango cha soka ilichokionesha stars katika mchezo huo hapo jana.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na kisima cha habari katika mtandao huu wapenzi na mashabiki wa soka wamesema kuwa, hivi sasa wanamatumaini makubwa na kikosi cha stars kutokana na michezo timu hiyo iliyocheza huku ikionesha kiwango kizuri na kwamba Stars inaweza kwenda mbali endapo mipango endelevu juu ya timu hiyo ikiendelea kutiliwa mkazo.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Mbeya, mmoja wa mashabiki wa soka, Alex Mkelemi, amesema  kuwa kiukweli Stars hivi sasa inaonesha kuendelea kuimarika siku hadi siku na kuonesha kiwango kizuri licha ya kuwepo makosa madogomadogo kiufundi ambayo hata hivyo ameongeza kuwa mwalimu anaonekana kuyarekebisha kadri siku zinavyokwenda.


Picha ikionesha mchezaji wa stars na Ivory Cost kwenye hekaheka za kuwania tiketi ya kwenda Brazil hapo mwakani, ambapo Stars ililala 4-2, uwanja wa taifa Dar.

Kutokana na hali hiyo, Mkelememi ameongeza kusema kuwa dalili ya Tanzania kuanza kufanya vizuri katika medani ya soka ulimwenguni imeanza kuonekana ila kinachotakiwa ni kutilia mkazo mpango endelevu wa timu hiyo ikiwemo kuwekeza katika soka la vijana ambao ndio watakaokuwa askari wa kesho katika kikosi cha stars.

Naye John Ezekiel mwanafunzi wa chuo cha biashara CBE, Campus ya Mwanza, akizungumza na mtandao huu mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo hapo jana, alisema kuwa kuna mabadiliko makubwa katika kikosi cha Stars hivi sasa, kutokana na  uchezaji wa timu hiyo tofauti na miaka takribani kumi iliyopita.

Jonh alisema kuwa wachezaji wa stars hivi sasa wanajiamini wanaweza kumiliki mpira na kutengeneza nafasi na hatimaye kuzitumia vyema na kupata magoli, ingawa bado kuna hali Fulani ya kukosa uzoefu kitu ambacho wakiendelea kujengewa wanaweza wakafanya makubwa siku za usoni na hatimaye Tanzania kuondokana na kichwa cha mwendawazimu kunako medani ya soka.

Safari ya stars kuwania tiketi ya kuelekea huko nchini Brazil hapo mwakani katika fainali za kombe la dunia, iliishia njiani pale kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, baada ya kuvurugiwa mipango ya safari hiyo na tembo wa Ivory Cost kwa kufungwa mabao 4-2, huku stars ikianza kulisabahi lango la tembo hao dakika ya kwanza tu ya mchezo lililotiwa wavuni na Amri Kihemba na kuamsha hoihoi na ndelemo miongoni mwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo jumapili iliyopita.

Picha ikionesha umati wa watazamaji walijitokeza kuangalia mechi kati ya Stars na Ivory Cost uwanja wa taifa Dar.

Hata hivyo Ivory Cost ilisawazisha bao hilo na badae kuongeza la pili, lakini wakiwa hawajakaa sawa Stars ilisawazisha kupitia kwa Thomas Ulimwengu akiunganisha krosi nzuri kutoka kwa Shomari Kapombe.


Mambo yalibadilika na Ivory cost kuonesha uwezo wao kutokana na uzoefu walionao na hatimaye kufanikiwa kupata mabao mawili mengine na kuondoka uwanjani kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Stars katika mchezo huo.

Kwa matokeo hayo Ivory Cost imefanikiwa kuelekea huko nchini Brazil hapo mwakani baada ya kuongoza kundi lake kwa kuwa na pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika kundi lake huku Tanzania ikiendelea kuwa na pointi 6 huku ikibakiza mchezo mmoja na Gambia, na hivyo kufifisha matumaini ya kuendelea na harakati za kuwania tiketi ya safari ya kuelekea nchini brazil.