Wednesday 9 October 2013

MGOMO WA MABASI NCHINI TANZANIA






Mgomo  mkubwa wa mabasi ya abiria umeitikisa nchi na kuilazimisha serikali kusitisha kwa muda amri yake ya kuwatoza asilimia tano wasafirishaji wanaozidisha uzito.


Idadi kubwa ya mabasi ya abiria yanayofanya safari ndani na nje ya nchi yaligoma jumatatu hii katika miji mingi ya nchi na kusababisha taharuki kubwa kwa abiria waliokuwa wamekata tiketi kwa ajili ya safari zao.


Idadi kubwa ya abiria walipata wakati mgumu katika kituo kikuu cha mabasi jijini Dar es Salaam, Arusha na Moshi huku wasijue la kufanya.


Kulingana na taarifa kutoka katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi, wafanyakazi na mawakala wa mabasi mengi walikuwa wamesimama wakidai kuwa wamekatazwa na waajiri wao kuendelea na safari hadi watakapopewa maelekezo mengine.


Kufuatia hatua hiyo ya mabasi kugoma, kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, akizungumza jijini Dare es salam, alidai kuwa mgomo huo haukuwa halali kwa sababu wamiliki hao wa mabasi walikwisha kuingia mkataba na abiria kwa kuwauzia tiketi za kusafiria, hivyo hawakupaswa kuwanyima haki yao ya kusafiri.


Mpinga alisema kitendo cha kutowasafirisha abiria hao ni sawa na kuvunja sheria.


Hata hivyo, baada ya Kamanda huyo kukutana na viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), aliwataka wamiliki hao, hususan madereva kuwapeleka abiria hao kama tiketi zao zilivyokuwa zinaelekeza, huku akiagiza Sumatra kuwakamata wale wote watakaopinga kufanya hivyo na kuwanyang’anya leseni zao na hatua nyingine zichukuliwe dhidi yao.


Hata hivyo, amri hiyo iliongeza hasira, na kuzuka mvutano mkubwa uliozidisha taharuki miongoni mwa abiria.


Hali hiyo iliwafanya viongozi hao kuwasiliana tena na mamlaka za juu, na ndipo ilipokubaliwa kuyaruhusu mabasi yote kuondoka kwa masharti ya kutopimwa katika mizani.


Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Taboa, Severine Ngallo, alisema makubaliano yaliyofikiwa ya kusafirisha abiria yalikuwa ya muda, wakisubiri matokeo ya kikao ambacho kingefanyika jana kwa kuwakutanisha na viongozi wa serikali.


“Nawashauri abiria wasikate tiketi katika kipindi hiki kwani kuna uwezekano mgomo huo ukaendelea tena leo na siku nyingine endapo madai yetu ya kuondolewa tozo hiyo yatakataliwa,” alisema Ngallo.


Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema wizara imekubali kukutana na wasafirishaji hao, lakini akakana kuwapo kwa makubaliano ya mabasi kupita katika mizani bila ya kupimwa.


Nazo taarifa kutoka Jijini Arusha, mabasi yote yaligoma kuondoka kituo kikubwa cha mabasi kwa zaidi ya saa tatu, katika mwendelezo wa mgomo huo.


Hali hiyo ilimlazimu  Kamanda wa  Polisi mkoani humo, Liberatus Sabasi, kuingilia kati na kuwataka madereva hao kutumia busara ya kuendelea kuwasafirisha abiria wao ambao walikuwa tayari wameshawakatia tiketi.


Alisema kuwa kila abiria anapopanga safari yake ana kusudi lake, hivyo kuvunja safari kwa sababu za mgomo si busara.


Madereva hao walikubali kuendelea na safari kama kawaida majira ya saa mbili asubuhi huku wakidai kuwa hawajui mahali pa kuwapeleka abiria hao kwani mgomo wao ni wa nchi nzima.