Sunday 20 October 2013

HATUMWI MTOTO SOKONI LEO


Wachezaji wa Simba na Yanga wakisalimiana kabla ya moja ya mchezo msimu uliopita

Leo ndio leo, asemae kesho ni muongo.

·     Ni Simba au Yanga kutakata?
·     Polisi Dare es salaam yaimarisha ulinzi katika mchezo huo.

                           
                                   Na. Deo Kaji Makomba.


Ni patashika nguo kuchanika nyasi kuwaka moto jumapili hii ambapo vigogo vya soka nchini Tanzania Simba na Yanga, viko uwanjani kupepetana katika mchezo ambao unachukuliwa  umuhimu mkubwa na timu zote mbili.

Mchezo huo ni miongoni mwa mfulilizo wa mechi za harakati za kuwania ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Vodacom Tanzania bara,  unapigwa jioni hii, kwenye uwanja wa taifa jijini Dare es salaam.

Tayari homa ya mchezo huo imezidi kupanda miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa timu hizo, huku kila upande ukitaka kushinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye harakati hizo za kuwania ubingwa wa ligi kuu hiyo ya soka ya Vodacom Tanzania bara msimu huu.

Mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi Esrael Nkongo, unapigwa baada ya siku 52 tangu watani hao wakutane mara ya mwisho Mei 18, ambapo Yanga walishinda mabao 2-0 chini ya Kocha Ernie Brandts.
Mabao hayo ambayo yalipeleka faraja kubwa  kwa timu hiyo yenye masikani yake katika mitaa Twiga na  Jangwani katika mechi hiyo ya kufunga msimu wa 2012/13, yalifungwa na Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza.

Kipigo hicho kinaifanya Simba chini ya Kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni kuwa na deni la kufuta uteja kwa , huku Yanga wakitaka kushinda kuendeleza ubabe mbele ya watani wao wekundu wa msimbazi Simba.

Licha ya Yanga kushinda 2-0, bado inatamani kulipa kisasi cha mabao 5-0 cha Mei 6, 2012, hivyo mechi ya jumapili ya leo kuwa yenye ushindani mkubwa zaidi kwa kila moja kupigania ushindi.

 Picha ikionesha wachezaji wa Simba na Yanga wakipambana uwanjani katika msimu uliopita wa ligi kuu ya soka ya Vodacom Tanzania bara.

Timu hizi zinakutana huku Simba ikiwa ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 18, nyuma ya Azam na Mbeya City zenye pointi 20 kila moja, na Yanga nafasi ya tano ikiwa na pointi 15.

Wakati Simba ikiwa na hesabu za kurejea kwenye usukani kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoingia raundi ya nane tangu ilipoanza Agosti 24, Yanga watakuwa wakitaka kufuta pengo la pointi tatu baina yao.

Kocha msaidizi wa timu ya Yanga,  Fred Felix Minziro amesema, ukiondoa Salum Telela ambaye ni  majeruhi, wengine wote wapo katika hali nzuri.

Kwa upande wa Simba, Kocha msaidizi Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema vijana wao wapo vizuri kuwakabili Yanga  kwani kila mmoja yu fiti akisubiri kwa shauku kubwa kupangwa katika mpambano huo wa kukata na mundu.
 Zinapokutana Simba na Yanga huwa ni patashika. Picha ikionesha hekaheka miongoni mwa wachezaji wa Simba na Yanga katika kuwania mpira.

Mandalizi ya mchezo huo yanaelezwa kukamilika,  na shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, huku jeshi la polisi jijini Dare es salaam, likieleza kujidhatiti kiusalama zaidi katika mchezo huo ambapo kila timu hizo zinapokutana hukusanya mashabiki weng.

Viingilio vya mechi hiyo, ni sh 30,000 kwa viti vya VIP A; VIP B sh 20,000; sh 15,000 kwa viti vya VIP C; sh 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa; Bluu sh 7,000 na Kijani sh 5,000.