Monday 16 December 2013

WATU SABA WANASHIKILIWA NA POLISI MKOANI MWANZA KUFUATIA MAUAJI YA MWENYEKITI WA ZAMANI WA CCM MKOANI MWANZA, MAREHEMU MABINA.

Mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza,  marehemu Clement Mabina, maarufu kama Wembe, baada ya kupigwa na mawe hadi kufa na wananchi wenye hasira, katika kijiji cha Kanyama Bukelebe wilayani Magu mkoani Mwanza. 



Sakata la mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Mwanza marehemu Mabina, lachukua sura mpya.
·    Watu saba wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
·    Hofu yatanda miongoni mwa wakazi wa kijiji cha Kanyama, baadhi yao waelezwa kukimbia kuhofiwa kukamatwa na polisi.


Na. Baltazar Mashaka.

Watu saba wanashikiliwa na Polisi jijini Mwanza wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya kinyama ya aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza na Diwani wa Kata ya Kisesa, Clement Mabina,almaarufu Wembe.

Watu hao wamekamatwa wakati hofu ikiwa imewakumba wakazi wa maeneo ya Kisesa na Kanyama, eneo ambalo marehemu Mabina aliuawa na watu wenye hasira katika kile kilichoelezwa kuwa mgogoro wa mashamba.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP,Valentino Mulowola, akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu, alisema hadi sasa watu saba wanashikiliwa na jeshi hilo.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti jana,ambapo jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Mwanza.

“Tunaendelea na upelelezi wa tukio hili la mauaji ya kinyama  ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika na kuna maendeleo mazuri. Tuna washikilia watu saba wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo,” Alisema  SACP Mulowola.

Katika tukio hilo la mauaji, Mabina aliuawa kwa kukatwa mapanga na kupigwa mawe ambapo alikutwa na majeraha makubwa kichwani kichogoni.

Kabla ya kuawa na wananchi  hao,marehemu alimpiga risasi mtoto Temeli Malemi kwa (11) bahati mbaya wakati akijihami na mashambulizi ya wananchi hao.
Ilielezwa jana na Kamanda wa Polisi SACP Mulowola kuwa marehemu alikutwa na silaha mbili aina ya Short-gun na bastola moja.

Hata hivyo ndugu wa marehemu walishindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kuhusiana na habari zilizoandikwa na mitandao ya kijamii ikihusisha kifo cha Ndugu yao (Mabina) na masuala ya kisiasa.

Aidha habari kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema kuwa mmoja wa watuhumiwa waliokamatwa alikutwa na simu ya mkononi ya marehemu na hata hivyo kamanda hakutaka kutaja jina lake na watuhumiwa wengine kwa madai ya kuvuruga upelelezi.  
  
Uchunguzi uliofanywa na Kisima cha habari umebaini kuwa tayari hofu kubwa na taharuki imewakumba wakazi wa kijiji cha Kanyama na Bukelebe huku  baadhi yao wakielezwa kuyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa.