Monday 30 December 2013

ERNEST MANGU NDIYE KAMANDA MPYA WA JESHI LA POLISI NCHINI TANZANIA.>>>>>>>

Ernest Mangu, Mkuu mpya wa jeshi la polisi nchini Tanzania. ( Picha na maktaba yetu)


Rais Kikwete amteua Kamishina wa Polisi Ernest Mangu kuwa mkuu mpya wa jeshi hilo.
·    Kuapishwa jumanne hii  viwanja vya Ikulu Dar.
·    Nafasi ya naibu mkuu wa jeshi la polisi yaanzishwa.

Na. Ofisi ya Ikulu.

Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzanzania Jakaya Mrisho Kikwete leo jumatatu Desemba 30, 2013,  amemteua Kamishina wa Polisi Ernest Mangu kuwa Mkuu wa jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue inaeleza kuwa Kamishina Mangu anachukua nafasi ya mkuu wa Jeshi la Polisi nchini anayestaafu, Said Mwema.

Kabla ya uteuzi wake unaoaanza januari mosi 2014, Kamisha Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Intelijensia ya jinai (Director of Criminal Intelligence) katika jeshi hilo la polisi.

Aidha taarifa hiyo inasema kuwa Rais Kikwete amemteua Kamishina Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Mkuu wa wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania ikiwa ni nafasi mpya katika muundo wa sasa wa jeshi hilo.

Kabla ya uteuzi wake, Kamishina Kaniki alikuwa Kamishina wa Uchunguzi wa Kijinai (Commissioner  for  forensic Investgations.)

Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya ataapishwa jumanne hii Desemba 31, 2013 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano,
Ikulu.
Dar es Salaam.

WAFANYABIASHARA MWANZA WAITIKISA SERIKALI.>>>>>>>>>

Bw. Filip Chibululu almaarufu Mandela, akiwa ameshika bango, kama linavyojieleza hapo, kama alivyonaswa na kamera ya Kisima cha habari katika maeneo ya Mwanza hotel jana, wakati wafanyabiashara walipoanza mgomo wao.


Wafanyabiashara Mwanza waitikisa serikali.
·    Wagoma kufungua maduka kisa mashine mpya za kielektronik zinazohusiana na masuala ya kodi.
·    Walia na bei za mashine hizo.

Na. Baltazar Mashaka.

WAFANYABIASHARA na Matajiri wa Jijini la Mwanza, wameitikisa Serikali, wakipinga ununuzi wa mashine za Kielektroniki, Electronic Fiscal Device (EFD) na manyanyaso kutoka taasisi za umma .

Wafanyabiashara hao jana asubuhi, walianza mgomo na kutofungua maduka yao hadi hapo serikali itakapokutana na kukaa meza moja, ili kutafuta suluhu ya unyanyasaji wanaofanyiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), Halmashauri ya Jiji na Jeshi la Polisi mkoani hapa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Kisima hiki cha habari jijini Mwanza jana, wafanyabiashara hao walisema mgomo huo usio na kikomo utafikia mwisho baada ya serikali kuona umuhimu wa kukutana nao.

Walidai kuwa maofisa wa TRA wana wanyanyasa kwa kuwakadiria kodi kubwa kuliko wanapoingiza shehena ya bidhaa kutoka nje ya nchi, na wakati mwingine hutakiwa kupeleka nyaraka za mizigo hiyo Dar es salaam.

Pia wanadai kulazimishwa kununua mashine za EFD kwa bei kati ya sh. 800,000 hadi 1,000,000 ,wakati mashine hizo bei yake halisi haizidi sh.200,000 na kuhoji TRA wana maslahi gani na mashine hizo.

Malalamiko mengine ni dhidi ya  halmashauri ya jiji  kuwatoza ushuru wa mizigo wanayotoa stoo na kuingia dukani,huku polisi nao wakidaiwa kuwaomba stakabadhi kwa bidhaa zinazoingizwa dukani kutoka stoo.

“TRA,Jiji na Polisi wametugeuza shamba la bibi. Unapo crea mzigo mpakani bila kuwapa cha juu unakadiriwa kodi kubwa. Ukifika hapa wanadai aliyekagua mzigo amekosea ili mradi uwape hela. Halmshauri nao wanataka ushuru hata kwa bidhaa unazoingiza dukani, ni unyanyasaji tu.” Alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Walidai Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Mhandisi Evarist Ndikilo, pamoja na kuandikiwa barua na wafanyabiashara hao kupitia kwa Mwanasheria wao,wakimtaka akutane nao Desemba 20, mwaka huu,hakuwajibu badala yake akaenda kufanya siasa na waendesha pikipiki.

Kampuni ya Uwakili ya Kabonde na Magoiga, ilikiri kumwandikia barua Mkuu wa mkoa  ikimtaka akutane na wateja wao ili kujadili na kutafuta ufumbuzi malalamiko yao.

“Wateja wetu walitupa maelekezo yao na sisi tukamwandikia barua RC tukimtaka akutane nao Desemba 2013 mwaka huu, lakini alitujibu kwa barua yenye kumb BE 222/226/01/26 ya tarehe 27 Desemba. Tumeipokea saa 3:00 asubuhi wakati  tayari wateja wetu wakiwa wameanza mgomo,”alisema mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo kwa sharti la kutotajwa jina kwa vile si msemaji.

Alisema RC alipaswa kujibu barua hiyo kabla ya mgomo na kunusuru usumbufu na kero wanayopata wananchi, sababu  mgomo  huo  una athari kubwa kiuchumi kwa taifa na kijamii na pengine hakuona umuhimu wa wafanyabiashara hao kuhudumia  wananchi.

“Mkuu wa mkoa alifanya siasa badala ya kuangalia uchumi wa nchi na athari zake kutokana na mgomo wa wafanyabiashara hao. Hakuona umuhimu wake. Leo wananchi wanahangaika ukizingatia shule zinafunguliwa na wanafunzi wanamahitaji ya shule na mahitaji mengine muhimu ya  jamii.”Alisema.

Habari za uhakika kutoka ofisi ya RC zinasema, alikuwa akikutana na viongozi wa wafanyabiashara hao mchana huu kwenye ukumbi wa ofisi yake, kujadiili kadhia hiyo pampoja na malalamiko yao.

Kisima cha habari kilishuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamekusanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi cha Tanganyika, huku mitaa yote ya katikati ya jijiji maduka yakiwa yamefungwa, ukiondoa wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga ) ambao waliendelea kufanya biashara katika mtaa wa makoroboi na maeneo mengine.

Lakini si maeneo ya mjini kati tu, aidha eneo la Nyakato National pia lilionekana idadi kubwa ya maduka ikiwa imefungwa katika kile kilichoelezwa ni kuunga mkono mgomo huo  wa wafanya biashara.