Tuesday 19 November 2013

WAKAAZI WA MWANZA WAMZUNGUMZIA MTU ALIYEFANYA MAUAJI YA SILAHA DAR.

Marehemu Gabriel Munisi Masama, baada ya kuwapiga risasi watu wawili na kisha naye kujifyatua risasi jijini Dare es salaam.


Tukio la kuwapiga risasi na kuwauwa watu wawili Jijini Dar lapokelewa kwa hisia tofauti jiji Mwanza.
·    Kila mmoja azungumza lake kuhusiana na unyama huo.
·    Baadhi ya wakaazi jijini Mwanza waliokuwa wanamfahamu aliyetekeleza tukio, wanena.
·    Nyumbani kwa baba wa mzazi wa marehemu kwatokea kioja.

                                                               Na. Mwandishi wetu.

Tukio la kijana Gabriel Munisi  la kuwapiga na kuwauwa kwa risasi watu wawili na hatimaye naye kujipiga risasi na kisha kufa,  asubuhi ya jumanne hii jijini Dare es salaam, limepokelewa kwa hisia tofauti na wakaazi jijini Mwanza huku kila mmoja akizungumza la kwake kutokana na tukio hilo, lililomuhusisha muuaji ambaye alikuwa mkaazi na mzaliwa wa Mwanza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Kisima hiki cha habari jijini mwanza, wakaazi hao ambao hawakutaka majina yao kuwekwa wazi, wasema kuwa tukio hilo limewasikitisha sana kutokana na marehemu Gabriel Mushi, kuchukua hatua ya kutwanga risasi na kisha kuwauwa na kuwajeruhi watu kadhaa ambao hawakuwa na hatia katika eneo la Ilala Bungoni karibu na baa maarufu kwa jina la klabu ya wazee.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza katika maeneo ya Mwanza hotel, waakazi hao walisema kuwa Gabriel Munisi wakati wa uhai wake alianza kuwa mbabe huku akifanya baadhi ya matendo ambayo yalikuwa yakienda kinyume na haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kufanya fujo katika maeneo ya starehe na wakati mwingine kuwatishia silaha wenzake wakati wanapoitilafiana kwa njia moja ama nyingine.

Mmoja wa madereva wa tax anayeegesha katika maeneo ya Mwanza hotel, ambaye alitaka  jina lake lihifadhiwe alisema anamfahamu vizuri kijana Gabriel Munisi, ikiwa ni pamoja ubabe wake, na ndio maana hakutaka kabisa kuwa na mazoea naye.

“ Unajua bwana huyu dogo hivi karibuni alianza kuwa na kiburi sana, na kuwa mbabe hivi. Hata hivi karibuni tu hapa walikuwa wanadaiana pesa Fulani na madereva wenzetu wa tax hapa Mwanza hotel, lakini mkwara alioupiga pale ulikuwa ni wa kutisha hali aliyomfanya mmoja wa madereva hao kukimbilia benki na kuchukua pesa na kumlipa dogo.” Alisema dereva tax huyo.

 Mwili wa marehemu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota surf.

Mkaazi mwingine aliyezungumza na Kisima  hiki cha habari jijini Mwanza ni mwanadada anayefanya kazi Mwanza hotel.

Mwanadada huyo ambaye naye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa baada ya kupata taarifa kuhusiana na tukio hilo kwa upande wake alionesha kufurahia  kufa kwa kijana Gabriel Mushi maarufu kama Gabby Masama, lakini akasema ameumia watu wengine wasiokuwa na hatia kuuawa.

“Ndugu yangu huyu kijana hana maana kabisa, wacha afe tu, alikuwa na roho mbaya sana na kiburi.” Alisema mwanadada huyo na kuongeza kuwa, “ Siku moja tulikuwa zetu klabu Mwanza hotel tukinywa vinywaji na kuburudika naye tukiwa pamoja kama kijana tunayemfahamu na mwisho tukitaka kuelekea nyumbani usiku wa manane alisema atupe rift kwani alikuwa na gari alituchukua lakini aliyotufanyia Gabby sitasahau maishani mwangu, acha afe. Alisema dada huyo.

Mapema leo asubuhi milio ya risasi zaidi ya kumi ilisikika eneo la Ilala Bungoni karibu na baa maarufu ya Wazee (Club ya Wazee), watu watatu wakiripotiwa kufariki kutokana na tukio hilo linaloelezwa kuwa limetokana na wivu wa kimapenzi.

Dereva mmoja wa tax kituo cha Bungoni ambaye alikuwa shuhuda wa kwanza, alisema mapema leo asubuhi alipata mteja aliyehitaji kupelekwa sehemu, ila kabla hawajafika huko walipokuwa wanataka kwenda jamaa ambaye ndiye alikuwa ni muuwaji alimuomba akatishe safari na kumtaka ampeleke sehemu nyingine.

Kwa mujibu wake dereva huyo aliendelea kusimulia, alimpeleka jamaa mpaka aneo la tukio hilo kwenye nyumba iliyopo pembeni mwa Hotel mpya iitwayo MM.

Mara baada ya kufika hapo, jamaa alitoa sh. 5,000 na kumkabidhi dereva ila cha kushangaza ni kitendo cha jamaa huyo kutoa bastola wakati akiwa anaelekea kwenye geti la nyumba, aliendelea kusimulia dereva huyo.

Wakati jamaa anaelekea getini mlango ulifunguliwa na gari aina ya Toyota Surf ilitoka ikiwa na watu wanne ndani, mwanaume mmoja ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari mama mmoja na wadada wawili.

Jamaa akiwa na bastola alianza kuwashambulia watu waliokuwa ndani ya gari hilo na kumpiga risasi dereva na mdada mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Carol, hii ni kwa mujibu wa dereva huyo na mara baada ya kuona hivyo  ikabidi akimbie.

Vyanzo vingine vinaeleza kuwa katika tukio hilo jamaa pia limpiga risasi ya mgongoni mama wa mwanamke aliyemuua na pia alimpiga msichana mwingine risasi ya mguu.

Mtuhumiwa na dereva aliyekuwa akiendesha gari walifariki palepale huku msichana mmoja akielezwa kufariki akiwa njiani kuelekea hospitali.

Bado haijafahamika moja kwa moja chanzo cha mauwaji hayo licha ya watu wengi ambao nilipata bahati ya kuongea nao wakilihusisha tukio hilo na mambo ya kimapenzi.

Akizungumza na Kisima hiki cha habari kuhusiana na tukio hilo wakili maarufu jijini Mwanza Mutalemwa alisema kuwa anashangazwa na taratibu zinazotumika ili mtu kuweza kumiliki silaha.

Alisema imefika wakati sasa kuangalia upya sheria ya umiliki silaha nchini, kwani baadhi ya wamiliki wengi wao wamekosa elimu ya matumizi ya silaha na hivyo kusababisha matukio ya mauaji ambayo siku za hivi karibuni yamekuwa yakigonga vichwa vya habari.

Ikumbukwe kwamba hivi karibuni, mwandishi wa habari wa ITV na Radio one Ufoo Saro alinusurika kufa katika tukio la kupigwa risasi na mzazi mwenzie tukio lililosabisha vifo vya watu wawili akiwemo mama  mzazi wa mwandishi huyo, ikiwa ni miongoni mwa matukio ya matumizi mabaya ya silaha.

Na habari tulizozipata kutoka nyumbani kwa baba mzazi  wa marehemu Gabriel Munisi, mtaa wa Kitangiri jijini Mwanza,zinaeleza kuwa, baada ya kupata taarifa ya kifo cha kijana wake alifanya tukio ambalo liliwashangaza wakaazi wa eneo hilo pale alipofunga mbwa  kwenye geti la nyumba yake kwa kile kilichoelezwa na  mashuhuda wa tukio hilo kuwa ni kuwazuiya watu wasifike nyumbani kwake, hata hivyo  sababu za kufanya hivyo hazikuweza kufahamika.

No comments:

Post a Comment