Saturday 10 August 2013

MABINGWA WAPYA WA MEYA CUP JIJINI MWANZA HAWA HAPA

Mabingwa wapya wa Meya Cup 2013, timu ya soka ya Isamilo FC, kutoka kata ya Isamilo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wa mashindano hayo(Picha na Deo Kaji Makomba)


Timu ya kata ya Isamilo yaibuka mabingwa wa Meya Cup

·        Ni baada ya kuibenjua timu ya Mkolani FC kwa mikwaju ya penaiti.



·       Mashindano hayo kuwa ya kudumu

             
       Na. deo kaji makomba

Hatimaye mashindano ya kandanda ya kuwania kombe la Meya jijini Mwanza, maarufu kama Meya Cup, yamefikia tamati  jumamosi hii huku bingwa wa mashindano hayo akipatikana.

Timu ya kata ya Isamilo FC, imeibuka bingwa wa mashindano hayo baada ya kuibenjua timu ya soka ya kata ya mkolani kwa changamoto ya mikwaju ya penaiti 3-1 na hivyo kujinyakulia zawadi ya mshindi wa kwanza.

Katika mchezo huo ulipigwa kwenye uwanja mkongwe wa nyamagana jijini Mwanza ulishuhudiwa timu zote zikitoka uwanjani zikiwa zimefungana bao 1 -1, na hivyo mwamuzi wa mpambano huo, kuamua sheria ya mikwaju ya penaiti ichukue nafasi yake na hatimaye bingwa kupatikana.

Katika fainali hizo zilihudhuria na mamia ya mashabiki wa soka pamoja na viongozi mbalimbvali wakiwemo wa vyama na serikali.

Bingwa wa Meya Cup alizawadiwa Bajaji yenye thamani ya shilingi milioni Nne na pesa tasilimu shilingi 1,500,000, wakati mshindi wa pili akipata milioni tatu, nayo timu ya kata ya Mbugani ikichukuwa nafasi ya tatu na hivyo kujinyakulia zawadi ya shilingi laki tano.

Jumla ya timu 19 zilishiriki katika mashindano hayo, ambapo timu hizo zikitoka katika kata mbalimbali jijini Mwanza pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo timu ya Magazeti FC.

Kwa upande wake msitahiki meya wa halmashauri ya wilaya ya Nyamagana, Stanslaus Mabula, akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali ya mashindano hayo, amesema kuwa mashindano hayo yatakuwa ya kudumu huku lengo lake likiwa ni kuibua na kuendeleza  vipaji vya soka.



TUKIO LA KUIBIWA KWA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA LAZIDI KUWAPASUA VICHWA WAKAAZI JIJINI MWANZA.



 Ni kuhusiana na nyaraka mbalimbali pamoja na Laptop mbili zilizoibiwa.

·       Wahoji kulikoni jeshi la polisi kuibiwa?



·       Wataka kufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli kuhusu tukio hilo la wizi.

            Na. deo kaji makomba

Tukio la kubomolewa na kuibiwa vitu kadhaa ndani la jeshi la polisi mkoani Mwanza, limezidi kuwapasua vichwa na kuwachanganya wakazi wengi jijini Mwanza huku wakibaki  kujiuliza kulikoni Polisi akaibiwa?
Mshangao huo umejidhihirisha kuzidi kutanda katika vichwa vya watu wengi jijini Mwanza , mara baada ya mahojiano yaliyofanyika kwa nyakati tofauti jijini humu  kuhusiana na kutolewa kwa taarifa ya kuwa jeshi hilo katika kituo cha kati limeibiwa baadhi ya vitu zikiwemo komputa mbili aina ya laptop.

Wakizungumza katika mahojiano maalum na Kisima cha habari Jijini Mwanza wakazi wa jijini humo wamesema kuwa, tukio hilo limewasitua na kuongeza kuwa endapo kama walinzi wa usalama wa raia na mali zake wanaibiwa , basi maisha ya mtu wa kawaida yako hatarini kama si mashakani.

Akizungumza kwa sharti la kutokuwekwa jina  lake wazi ,mmoja wa wakazi wa jijini Mwanza, alisema kuwa tukio hilo linadhihirisha kuwa ndani ya jeshi la polisi huenda kuna askari hawana dhamira nzuri na jeshi hilo hivyo chochote kinaweza kutokea.

“Unajua mwandishi mambo mengine ni ya kuacha tu, hivi kweli inaangia akilini kuona polisi anaibiwa?” Alihoji mkazi huyo aliyesisitiza kutokuweka wazi jina lake.

Naye bwana Abubakari Hasani Seif mkazi wa Nera jijini Mwanza akizungumza na Kisima cha habari amesema kuwa ni jambo la kusikitisha na la aibu na fedheha kama nyaraka ama vitu vinaweza kuibiwa ndani ya jeshi la polisi.

Amesema kuwa tukio hilo limetia shaka  utendaji ndani  jeshi la polisi na hivyo kupoteza imani kwa wananchi kuhusiana na utendaji mzima wa jeshi hilo.

Bwana Abubakari ameongeza kusema kuwa haiwezekani kitu kuvuja nje kama polisi ni wasafi, na kwamba kuna namna ndani yake kutokana na tukio hilo la wizi.

Aidha bwana Abubakari ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa Nera ameitaka serikali kuliangalia kwa umakini suala hilo hasa kutokana na baadhi ya ofisi za jeshi hilo kabati zake za kuhifadhia majalada mbalimbali ni chakavu na haziko katika hali ya usalama.

Kwa upande wake jeshi la polisi mkoani Mwanza, limesema kuwa bado liko katika uchunguzi ili kubaini kinagaubaga wale wote waliohusika na hatimaye sheria ichukue mkondo wake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Kisima hiki cha habari jijini Mwanza, kamanda wa polisi mkoani Mwanza Bwana Ernest Mangu, amesema kuwa wakaazi jijini Mwanza wanapaswa kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na usalama wao kwani jeshi hilo limejidhatiti kudhibidi hali ya uharifu mkoani humo.

Akizungumzia tukio liliotokea hivi karibuni la kubomolewa na kuibiwa baadhi ya vitu ikiwemo komputa mpakato moja (Laptop), kamanda Mangu  amesema kuwa uchunguzi wa awali ndani la jeshi hilo umeonesha waliohusika katika wizi huo ni raia na si polisi, ingawa hakutaja majina ya watu wanoshikiliwa kutokana na tukio hilo.

Alipoulizwa na Kisima cha habari imewezekanaje hadi wezi wakaingia katika eneo la kituo na kuboa sehemu ndani ya kituo na kasha kuiba baadhi ya vitu, kamanda Mangu alisema tukio hilo linatokana tatizo la kimipaka lililokuwepo katika eneo la kituo cha polisi kati kuingiliana na baadhi ya ofisi nyingine.

Kamanda Mangu ameongeza kuwa hata wezi walioiba hawakujua kama wanaiba katika kituo cha polisi. “Hivyo tumezibiti mipaka yote katika eneo la kituo cha kati na pia tunaendelea na uchunguzi wetu.” Alisema Kamanda Mangu.

Usiku wa kuamkia Julai 19 mwaka huu, watu wasiofahamika waliingia katika ghara la kuhifadhia nyaraka na vielelezo na nyaraka katika kituo kikuu cha polisi kati wilaya ya Nyamagana baada ya kuvunja dirisha za ofisi za ukaguzi kanda ya ziwa na kupora komputa mpakato mbili, ambazo zilikuwa ni vielelezo na nguo kama kielelezo cha kesi na kitabu cha kumbukumbu ya matukio na kasha kutokomea kusikojulikana.