Ni kuhusiana na nyaraka mbalimbali pamoja na Laptop mbili zilizoibiwa.
· Wahoji kulikoni jeshi la polisi kuibiwa?
· Wataka kufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli kuhusu tukio hilo la wizi.
Na. deo kaji makomba
Tukio la kubomolewa na kuibiwa vitu kadhaa ndani la jeshi la
polisi mkoani Mwanza, limezidi kuwapasua vichwa na kuwachanganya wakazi wengi
jijini Mwanza huku wakibaki kujiuliza
kulikoni Polisi akaibiwa?
Mshangao huo umejidhihirisha kuzidi kutanda katika vichwa
vya watu wengi jijini Mwanza , mara baada ya mahojiano yaliyofanyika kwa
nyakati tofauti jijini humu kuhusiana na
kutolewa kwa taarifa ya kuwa jeshi hilo katika kituo cha kati limeibiwa baadhi
ya vitu zikiwemo komputa mbili aina ya laptop.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na Kisima cha habari
Jijini Mwanza wakazi wa jijini humo wamesema kuwa, tukio hilo limewasitua na
kuongeza kuwa endapo kama walinzi wa usalama wa raia na mali zake wanaibiwa ,
basi maisha ya mtu wa kawaida yako hatarini kama si mashakani.
Akizungumza kwa sharti la kutokuwekwa jina lake wazi ,mmoja wa wakazi wa jijini Mwanza,
alisema kuwa tukio hilo linadhihirisha kuwa ndani ya jeshi la polisi huenda
kuna askari hawana dhamira nzuri na jeshi hilo hivyo chochote kinaweza kutokea.
“Unajua mwandishi mambo mengine ni ya kuacha tu, hivi kweli
inaangia akilini kuona polisi anaibiwa?” Alihoji mkazi huyo aliyesisitiza
kutokuweka wazi jina lake.
Naye bwana Abubakari Hasani Seif mkazi wa Nera jijini Mwanza
akizungumza na Kisima cha habari amesema kuwa ni jambo la kusikitisha na la
aibu na fedheha kama nyaraka ama vitu vinaweza kuibiwa ndani ya jeshi la
polisi.
Amesema kuwa tukio hilo limetia shaka utendaji ndani jeshi la polisi na hivyo kupoteza imani kwa
wananchi kuhusiana na utendaji mzima wa jeshi hilo.
Bwana Abubakari ameongeza kusema kuwa haiwezekani kitu kuvuja
nje kama polisi ni wasafi, na kwamba kuna namna ndani yake kutokana na tukio
hilo la wizi.
Aidha bwana Abubakari ambaye pia ni mwenyekiti wa mtaa wa
Nera ameitaka serikali kuliangalia kwa umakini suala hilo hasa kutokana na baadhi
ya ofisi za jeshi hilo kabati zake za kuhifadhia majalada mbalimbali ni chakavu
na haziko katika hali ya usalama.
Kwa upande wake jeshi la polisi mkoani Mwanza, limesema kuwa
bado liko katika uchunguzi ili kubaini kinagaubaga wale wote waliohusika na
hatimaye sheria ichukue mkondo wake.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Kisima hiki cha
habari jijini Mwanza, kamanda wa polisi mkoani Mwanza Bwana Ernest Mangu,
amesema kuwa wakaazi jijini Mwanza wanapaswa kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na
usalama wao kwani jeshi hilo limejidhatiti kudhibidi hali ya uharifu mkoani
humo.
Akizungumzia tukio liliotokea hivi karibuni la kubomolewa na
kuibiwa baadhi ya vitu ikiwemo komputa mpakato moja (Laptop), kamanda Mangu amesema kuwa uchunguzi wa awali ndani la jeshi
hilo umeonesha waliohusika katika wizi huo ni raia na si polisi, ingawa hakutaja
majina ya watu wanoshikiliwa kutokana na tukio hilo.
Alipoulizwa na Kisima cha habari imewezekanaje hadi wezi
wakaingia katika eneo la kituo na kuboa sehemu ndani ya kituo na kasha kuiba
baadhi ya vitu, kamanda Mangu alisema tukio hilo linatokana tatizo la kimipaka
lililokuwepo katika eneo la kituo cha polisi kati kuingiliana na baadhi ya
ofisi nyingine.
Kamanda Mangu ameongeza kuwa hata wezi walioiba hawakujua
kama wanaiba katika kituo cha polisi. “Hivyo tumezibiti mipaka yote katika eneo
la kituo cha kati na pia tunaendelea na uchunguzi wetu.” Alisema Kamanda Mangu.
Usiku wa kuamkia Julai 19 mwaka huu, watu wasiofahamika
waliingia katika ghara la kuhifadhia nyaraka na vielelezo na nyaraka katika
kituo kikuu cha polisi kati wilaya ya Nyamagana baada ya kuvunja dirisha za
ofisi za ukaguzi kanda ya ziwa na kupora komputa mpakato mbili, ambazo zilikuwa
ni vielelezo na nguo kama kielelezo cha kesi na kitabu cha kumbukumbu ya
matukio na kasha kutokomea kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment