Sunday 29 December 2013

RAGE BADO NI MWENYEKITI HALALI WA SIMBA.>>>>>>>>>

Mwenyekiti halali wa Klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba, Ismail Aden Rage.


Rage ndiye mwenyekiti halali wa Simba.
·    Maamuzi yaliyochukuliwa na kamatia ya utendaji ya Simba kumsimamisha yaelezwa ni batili.
·    Agizo la TFF kumtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa wanachama bado lipo palepale.
·    Nalo sakata la Okwi, TFF ladai kulitambua.

Na. Deo Kaji Makomba.

Ismail Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.

Kauli hiyo ya Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji inakuja kufuatia kubaini  mapungufu kadhaa ya kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao, katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jumamosi iliyopita jijini Dar es salaam.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF, na kusambazwa na ofisa habari wa Shirikisho hilo, Boniface Mgoyo Wambura na kasha nakala yake kukifikia Kisima cha habari, imebainisha  Upungufu huo kuwa  ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.

Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.

Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale.

Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.

Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.

TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.

Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.

Ama kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.

Wakati huo huo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.

Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.

Baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.

Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.

Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.

No comments:

Post a Comment