Tuesday 17 December 2013

RAIS KIKWETE AMTUMIA SALAM ZA RAMBIRAMBI MKUU WA MKOA WA MWANZA, KUFUATIA MAUAJI YA MWENYEKITI WA ZAMANI WA CCM MABINA NA TENERY MALIMI WAKATI WA VURUGU ZA ARDHI KITONGOJI CHA KANYAMA KISESA

Picha ikionesha mwili wa mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoani Mwanza, marehemu Clement Mabina, aliyepigwa kwa mawe hadi kufa jumapili iliyopita.



TAARIFA KUTOKA IKULU.

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amemtumia salam za rambirambi, mkuu wa mkoa wa Mwanza Eng. Evarist Ndikilo kufuatia vifo vya watu wawili vilivyotokea decemba 15 2013, katika kitongoji cha Kanyama Bukelebe kata ya Kisesa wilayani Magu, mkoani Mwanza.

Rais Kikwete ametuma salam  hizo kwa  mkuu wa mkoa wa Mwanza,kufuatia vifo vya Bw. Clement Mabina na Tenery Malimi vilivyotikea baada ya vurugu zilizosababishwa na mabishano ya ardhi.

Rais amemuomba mkuu wa mkoa huo, kuwatahadharisha wananchi kutochukua sheria mikononi mwao na pia kuwa waangalifu na matumizi ya silaha za moto.

“Nimesikitishwa na kufadhahishwa sana na taarifa za vifo vya wananchi hao wawili (2) vilivyosababishwa na mgogoro wa ardhi ambao ungeweza kupata suluhu kwa njia za amani. Ni vyema wananchi kuwa na subira na kuwa waangalifu katika kutatua migogoro yao.” Rais amesema na kuongeza kuwa “ ni vyema subira na busara zikawa ndio muongozo wa kutatua migogoro yetu katika jamii badala ya hasira”.

Aidha , Rais Kikwete amemuomba mkuu wa mkoa wa Mwanza,amfikishie salam za dhati kwa  kwa familia na ndugu wa marehemu Mabina pamoja na  Tenery Malimi, ambao walifariki kutokana na vurugu hizo.

“Amewaomba familia zote mbili ziwe na subira wakati huu mgumu kwa kuondokewa na wapendwa wao na kuviacha vyombo vya dola kuchukua hatua kwa kufuata taratibu zilizopo”. Kwa ndugu Mabina , Chama cha mapinduzi kimepoteza  mmoja wa viongozi wake mahiri na wakutumainiwa. Aidha, kwa marehemu Tenery, taifa limepoteza mmoja wa vijana wake wanaochipkia ambae angejaliwa kuishi angeweza kutoa mchango muhimu kwa maendeleo ya jamii na nchi yetu”.

Mabina amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo Diwani na mwenyekiti wa Halmashauri ya Magu mwaka 2000 hadi 2005, mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza, mwaka 2007 hadi 2012.

Rais ameziombea nyoyo za marehemu wote Mungu azilaze mahali pema peponi Amen.

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
DAR ES ALAAM.

No comments:

Post a Comment