Sunday 17 November 2013

PPF YATAKA MAKAMPUNI KUWASILISHA MICHANGO YA WANACHAMA KWA WAKATI.

Meshack Bandawe, meneja wa PPF kanda ya ziwa.


PPF yayaonya makampuni yanayoshindwa kuwasilisha michango ya watumishi kwa wakati.

                            Na. Mwandishi wetu.

MFUKO wa Pensheni wa PPF, umeyaonya Makampuni yanayoshindwa kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati kwenye mifuko ya hifadhi yaache tabia hiyo, vinginevyo yatafikishwa mahakamani .

Onyo hilo limetolewa jana Jijini Mwanza na Meneja wa PPF, Kanda ya Ziwa ,Meshach Bandawe, wakati akifunga mafunzo ya askari wa kampuni binafsi ya ulinzi ya KK Security.

Alisema ipo changamoto kubwa kwa baadhi ya makampuni ya ulinzi nchini, kutoandiskisha wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi,hata wanapowaandikisha inakuwa vigumu kuwasilisha michango yao kwa wakati.

Alisema hali hiyo inasababisha wafanyakazi hao kuhangaika mara wanapotoka kwenye ajira kwasababu mbalimbali.

“Nitoe onyo kwa makampuni ya namna hiyo kutoendelea na tabia hiyo na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ili kulinda maslahi ya wafanyakazi.Katika hili tayari mfuko wa PPF tumefungua mashauri mahakamani kwa baadhi ya makampuni ya ulinzi yanayoshindwa kuwasilisha michango ya wanachama wetu, ”alisema Bandawe.


 Picha ikionesha askari wa moja ya makampuni binafsi ya ulinzi wakiwa katika mafunzo ya ulinzi na usalama.

Alisema changamoto nyingine ni mishahara midogo wanayolipwa watumishi hao wa makampuni ya ulinzi na licha ujira huo mdogo lakini pia hawalipwi kwa wakati, na kusababisha waishi kwa shida na familia zao,lhali wanafanya kazi kwenye mazingira magumu.

“Mazingira haya yanahuzunisha na kukatisha tamaa na kuzusha migogoro  isiyo ya lazima kati ya waajiri na wafanyakazi. Pia, hupunguza kiwango cha  uaminifu kwa walinzi hao,maana askari asiyelipwa ipo hatari ya kupoteza uaminifu na baaadhi kujiingiza kwenye vitendo uhalifu wanapoteekeleza majukumu yao,”alisema.

Aidha Bandawe aliwapongeza wafanyakazi wa KK Security kwa uamuzi wao sahihi wa kujiunga na mfuko huo na kuwahakikisha kupata huduma bora ya mafao mbalimbali, pamoja na kulipwa ndani ya siku saba baada ya kutoka kwenye ajira.

Pia alisema KK Security ni kampuni ya kuigwa kati ya makampuni ya ulinzi, kwani imeandikisha watumishi wake 6,285 kwenye mfuko wa PPF, ambapo imelipa bila kukosa michango ya watumishi inayofikia shilingi milioni 267,771,967.

Bandawe alisema kwa Kanda ya Ziwa, KK Security imeandikisha watumishi wapya 533 kwenye mfuko wa PPF kwa mwaka huu,hivyo akatoa rai kwa makampuni mengine nchini kutoka sekta zote za ajira ikiwemo ya umma,Serikali Kuu,Serikali za Mitaa,Sekta binafsi ,Taasisi zisizo za Kiserikali na sekta isiyo rasmi,kujiunga na mfuko huo ili wapate huduma bora na mafao bora.

Alisema mfuko wa PPF ndio pekee nchini,unaotoa mafao ya elimu kwa wanachama wake, kwa kusomesha watoto wao wasozidi wanne kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, inapotokea mwanachama amefariki.

Pia mfuko huo wa PPF unaoa mikopo ya gharama nafuu kupitia Saccos sehemu za kazi, na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zinazokopeshwa wanachama kuwawezesha kumiliki nyumba baada ya kustaafu.

Alisema kampuni ya KK Security imekuwa mstari wa mbele kuisadia serikali na jeshi la polisi kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na Taifa .

“Sote tunafahamu kwani bila usalama madhubuti ni vigumu sana kupata maendeleo ya ,ama yakipatikana  yanakuwa siyo ya kuridhisha.Bado pia jeshi la Polisi halina uwezo wa kumlinda kila mwananchi,kweu nyinyi kusaidia serikali mnakuwan mmetimiza wajibu wetu wa kulinda raia na mali zao,”alisema Meneja huyo wa PPF

No comments:

Post a Comment