Wednesday 4 December 2013

KATIKA MICHEZO: JK NA SOKA LA BONGO.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, akihutubia kwenye uwanja wa CCM Kirumba wakati alipopokea kombe la soka la dunia hivi karibuni jijini Mwanza.





JK alitwisha zigo TFF.
·    Aitaka Stars ishiriki kombe la dunia.
·    Asema TFF iondokane na migogoro na kuwekeza zaidi katika soka la vijana.

                 
                                Na. Baltazar Mashaka.

Rais Jakaya Kikwete, ameuonya Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), kutowekeza kwenye migogoro na maslahi binafsi,badala wawekeze kwenye soka na kuendeleza vipaji ili kuinua mchezo huo.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Ijumaa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, wakati akipokea kombe halisi la Dunia la FIFA,ikiwa ni  mara ya kwanza kupokelewa nje ya Dar es salaam na mara ya tatu kutinga hapa nchini.

Alisema uongozi wa TFF uone umuhimu wa kujipanga kwa kuimarisha vyama vya soka vya wilaya, mikoa na vilabu, kwani bila kuwa na vilabu imara ni vigumu kupata wachezaji bora wa timu ya Taifa.

Mkuu huyo wa nchi alisema viongozi wa TFF  wasitumie muda mwingi kuwekeza kwenye maslahi binafsi na migogoro isiyo na tija kwenye soka,sababu migogoro inadumaza maendeleo ya mchezo huo.

“Tunatumia muda mwingi kuwekeza migogoro na maslahi binafsi,acheni hayo muwekeze kwenye soka na kuendeleza vipaji na muanzishe vitalu (Academy ) vya watoto wadogo kwa manufaa ya baadaye,”alisema JK

Pia aliutaka uongozi huo kuacha kufungia wachezaji wanaokosa kwa kipndi kirefu, kwani kufanya hivyo kunasababisha wachezaji wasipate maendeleo ya kisoka.

“Ninapo wasema mnanuna,mnataka niwasifie tu,sasa badilikeni na muache kuwafungia miezi sita wachezaji wanaokosa !Kumfungia mchezaji muda huo hawezi kuendelea.Angalieni wenzetu Ulaya wao wanahesabu mechi,ninyi hapa mnawafungia miezi sita,” alisema JK na kuongeza;

“Malinzi,usiwe rais wa kutoa adhabu ya kufungia wachezaji waliokosa,lazima mbadilike.Wekezeni katika soka ya watoto,mtembee hadi vijijini kama ninavyofanya mimi,ikiwzekana anzisheni Academy zenu.” 

Kuhusu kombe hilo la FIFA, alisema ujio wake hapa nchini ni deni kwa uongozi wa TFF na unapaswa walilipe.Hivyo akalitaka shirikisho hilo kujipanga na kuhakikisha Tanzania inashiriki fainali za kombe la Dunia siku za usoni, ili Rais ajaye aweze kulishika kikweli kweli kombe hilo. 

“FIFA kwa kutembeza kombe hili,ujumbe wake unatutaka na sisi tuonekane kwenye fainali za kombe hilo.Ujumbe wangu kwa TFF, viongozi mkilala na kuamka,mfikirie kuendeleza soka,wachezaji,wapenzi na vilabu vya mchezo huo.Lakini pia ujio wa kombe hili ni deni kwenu, lazima mlilipe kwa kuinua kiwango cha mpira ili tushiriki fainali za kombe hilo,”alisema Rais

Alieleza kuwa ushiriki wetu wa timu ya Taifa kwenye fainali za kombe la Dunia unawezekana, na kuhoji mbona wenzetu barani Afrika wanaweza,kwa nini sisi ? Aliutaka uongozi wa TFF kweenda kujifunza kwao na ni muda muafaka wa kujipanga.

Alisema kuwa,akiwa katika ziara barani Ulaya aliwahi kukutana na Rais wa FIFA,Seppt Blatter,akamwuliza Tanzania tuwasaidieje katika kuinua mchezo wa soka?

“Niliwahi kukutana na Rais wa FIFA ambaye ni rafiki yangu,aliniuliza Tanzania tuwasaidieje ili muinue mpira wenu.Hebu TFF jipangeni,sababu serikali inawaunga mkono.Nilimleta Maximo, kocha wa timu ya Taifa,mshahara nilikuwa namlipa mimi,hata wa sasa mshahara namlipa mimi,”alisema.

No comments:

Post a Comment