Sunday 6 October 2013

NI MAJANGA KWA VILABU VYA TOTO NA PAMBA VYA MWANZA.



 Kikosi cha timu ya Toto African ya Mwanza, kilichoshiriki ligi kuu mwaka jana. Timu hiyo iko katika harakati za kutaka kurejea ligi kuu msimu ujao.(Picha na maktaba ya Kisima cha habari)

 Matumaini ya timu za Toto na Pamba kutaka kurejea ligi kuu ya soka ya Vodacom hapo mwakani yafifia


  •   Ni baaada ya kufanya vibaya katika mechi za ligi soka daraja la kwanza

  •  Wadau wa soka Mwanza wakitupia lawama chama cha soka mkoani Mwanza, MZFA                  

                                     
                                  Na. Mashaka Baltazar, Mwanza.


UNAWEZA Kusema kwa lugha rahisi na nyepesi kuwa haya ni majanga,baada ya kufifia kwa matumaini ya timu za Toto African na Pamba za Jiji la Mwanza, kufuzu kucheza Ligi Kuu ya soka ya Vodacom katika msimu ujao hapo  mwakani.





Matumani ya timu hizo yamezidi kufifia baada ya kushindwa kufanya vizuri katika michezo yake mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Toto waliokuwa nyumbani kwenye uwanja wa CCM Kirumba,kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya vinara wa ligi hiyo,Kanembwa JKT ya Kigoma.





Wakati hali ikiwa hivyo kwa Toto, Pamba nayo iliangukia pua baada ya kuchapwa  katika mechi iliyofanyika kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.





Kabla ya mechi hiyo Pamba ilikuwa imekubali kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa timu ngeni ya Stendi United ya Shinyanga kwenye uwanja wa CCM Kirumba,hali inayotoa mweleko kuwa timu hizo za Mwanza hazina nafasi tena ya kufuzu kwenye ligi hiyo.





Baadhi ya wadau wanaulaumu uongozi wa soka mkoani hapa kutokuwa na mikakati kama iliyopo kwa vyama vingine ya soka, hivyo ni ndoto za alinacha kuweza kuvusha timu kwenda Ligi Kuu hapo mwakani.





Walisema Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), kimekosa dira na mipango ya soka na kuhoji mikoa kama Shinyanga ama Kigoma inawezaje kufanya vizuri halafu Mwanza ishindwe ?





Walidai kuwa pamoja na Pamba kuonekana inaungwa mkono na Serikali ya mkoa kuliko Toto, ni wazi haina watu wa mipango na fitna ya soka. Lakini laiti Toto ineungwa mkono kama ilivyo Pamba ni dhahiri ingeweza kuonesha maajabu.





Hadi sasa Toto ina pointi nne baada ya kucheza mechi nne na kupoteza miwili kushinda mmoja na kutoka sare mchezo mmoja. Kadhalika Pamba imeshinda mechi moja, kutoka sare moja na kupoteza mmoja.





Viongozi wa MZFA hawakupatikana kuzungumzia mstakabali wa timu hizo za Mwanza, baada ya simu ya Mwenyekiti Jackson Songora kutokuwa hewani kila  ilipopigwa na mwandishi wa habari hizi.





No comments:

Post a Comment