Sekeseke la uchaguzi mkuu wa TFF.
· Nyalla,Nyaulingo, Nyenzi washinda rufani.
· Kamati ya rufani ya uchaguzi yawakuta hawana hatia.
· Sasa kushiriki Uchaguzi wa TFF octoba 27
Na. Mwandishi wetu, Dare es salaam.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro
cha uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka
huu jijini Dar es Salaam.
Samwel
Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo
inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga
uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote
wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali.
Akisoma uamuzi huo ijumaa hii mbele ya Waandishi wa Habari kwenye ofisi za
TFF, jijini Dare es salaam, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za Mrufani
Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;
Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya
ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na
ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.
Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu
fomu hiyo ya uongozi imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa ni vizuri fomu za
kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.
Kwa
vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa
mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona
itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile
tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.
Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu
yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15
kinachohusu malengo ya mgombea uongozi.
Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa
uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya
9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani
na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu
zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya
michezo kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki
wake kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na
ligi nyingine za kitaifa.
Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye
utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo,
Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na
amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.
Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama
mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika
uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka
mitano.
Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na
Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.
Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu
kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya
Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;
Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya
kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa
kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa
kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho
vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia
unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya
hivyo.
Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1
iliyojazwa na kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika
nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu
unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na
Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).
Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na
Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.
Wakati huo huo,
Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana jumapili hii, kufanyia mapitio
(revision) ya uamuzi wa Kamati ya Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama
ilivyoombwa na Sekretarieti ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.
No comments:
Post a Comment