Monday 12 October 2015

WAZIRI KIGODA HATUKO NAYE TENA






                        Aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara Abdalah Kigoda

WAZIRI KIGODA AFARIKI DUNIA HUKO INDIA.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda amefariki dunia leo saa 10 jioni nchini India alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila amethibitisha taarifa hizo, na kusema kuwa Dkt Kigoda alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Apollo, New Delhi na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Kwa mujibu wa kaka wa marehem Sadiki Kigoda aliyezungumza na na vyombo vya habari siku chache zilizopita, alisema kuwa Dkt Kigoda alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi.


 

STARS HIYOOO!

 
      Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa stars, kilichopambana huko Malawi

HEKA HEKA ZA KUWANIA KUPANGWA KWENYE MAKUNDI YA TIKETI ZA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA.
  •     Licha ya kufungwa bao 1-0 na Malawi, Stars yafuzu hatua ya pili 
                                  Na. Mwandishi wetu

Tanzania imeweza kutimiza ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya kufungwa 1-0 na Malawi jumapili iliyopita, katika Uwanja wa Kamuzu mjini Blantyre.

Tanzania inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya Jumatano iliyopita kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilifungwa na John Banda dakika ya 42 aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Chiukepo Msowoya.

Taifa Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu, mshambuliaji Mbwana Samatta alikaribia kufunga, baada ya kumtoka beki Limbikani Mnzava, lakini kipa Simplex Nthala akaokoa.

Malawi wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya shuti kali la Banda kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’. Barthez akafanya kazi nzuri tena dakika ya 10 baada ya kuokoa michomo miwili mfululizo ya Malawi.

Stars ilizinduka dakika ya 35 baada ya Thomas Ulimwengu kumtoka vizuri beki wa Malawi Yamikani Fodya baada ya pasi ndefu ya Samatta, lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko, akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John Bocco.

Mabadiliko hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo la Malawi, lakini bado mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa Tanzania.

Dakika ya 58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliokoa hatari langoni mwake na dakika ya 62 Malawi walifanya mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni mwa Stars, ikiwemo kupata kona mbili.

Dakika ya 72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.

Malawi walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo mwezi Novemba.

Kikosi cha Tanzania; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Said Ndemla/John Bocco dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Mrisho Ngassa dk75.

Malawi; Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Miracle Gabeya/Robin Ngalande dk76, Yamkani Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri, Chimango Kayira, Micium Mhone, Chiukepo Msowoya, John Banda na Shumaker Kuwali.